Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mhe.Twaha Mpembenue akiwa ameambatana na viongozi wa Chama na Serikali wa Wilaya ya Kibiti amezindua rasmi ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kata Mbuchi katika kijiji cha Mbwera Magharibi ambapo ujenzi utaanza hivi karibuni.
Katika uzinduzi huo Mhe. Mbunge amewapongeza wakazi wa Mbuchi kwa namna walivyojitoa kushiriki katika zoezi hilo pia ameahidi kushirikiana kwa dhati na Wananchi wa eneo hilo kwa lengo kuihudumia jamii na kuleta maendeleo.
Akizungumzia suala la ujenzi, Mpembenue amesema, wakati wowote kuanzia sasa ujenzi utaanza kwani vifaa vyote vipo tayari pamoja na mafundi.
Katika hafla hiyo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Meja Edward Gowele akatoa agizo kwa Mkurugenzi Mtengaji Mohamed Mavura na Mwnyekiti wa Halimashauri ya Wilaya ya Kibiti Ramadhani Mpendu kuhakikisha ujenzi wa sekondari hiyo unakamilika kwa wakati muafaka.
Pia Meja Gowele akawataka wazazi kusimamia malezi ya watoto kuhakikisha wanasoma na kuepukana na utoro,mimba na ndoa za utotoni huku akiwasihi wananchi kuendelea kujitolea panapohitajika kwani nguvu kazi ya wananchi ni muhimu katika kuleta maendeleo.
Vilevile Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ramadhani Mpendu, Mbunge, Madiwani na wadau wengine katika kuhamasisha ujezi huo wamefanya harambee fupi na kupata jumla ya shilingi 580,000 ili kuhakikisha wakazi wa Mbwera Magharibi wanapata shule kwa wakati.
Nae Mkurugezi Mtendaji Mohamed I. Mavura akawapongeza wakazi wa Mbwera Magharibi kwa jinsi wanavyojitolea kwa mambo ya maendeleo na kuwaahidi kuwa ,Serikali itawaunga mkono pale nguvu ya wananchi itakapoishia kuhakikisha ujenzi unakamilika.
Aidha Mwenyekiti wa CCM Wilaya Juma Ndaruke aliunga mkono jitihada za mhe. Mbunge na kuahidi kushirikiana na uongozi wa Chama na Serikali ili kuhakikisha Wilaya ya kibiti inapata maendeleo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.