8.4.2024
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Ndg, Rashid Mchatta amewataka wananchi kuishi kwa tahadhali na kufuata maelekezo ya wataalam wa Mazingira hasa katika kipindi hiki ili kuweza kujihami na maafa ambayo yanaweza kutokea.
"Poleni sana kwa Mafuriko haya, tumekuja na tumejionea hali halisi, nawapongeza sana kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoka katika maeneo yaliyozingirwa na maji mmepunguza kutokea kwa maafa" Alisema Mchatta.
Mchatta amesema hayo tarehe 8.4.2024 alipowasili katika Kitongoji cha cha Mtunda A mjini Kata ya Mtunda, katika ziara maalum ya kuwatembelea na kuwajulia hali wahanga wa Mafuriko ya maji yanayotokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha na kusababisha kufurika kwa mto Rufiji.
Vilevile Mchatta amewataka wananchi hao kuhakikisha wanatunza vizuri mazao waliyonayo kwa ajili ya kujiwekea akiba ya chakula kwani haijulikani janga hilo litachukua muda gani kuisha kwasababu mvua bado zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewataka wananchi kuchukua tahadhali kwa kuhamia katika maeneo yenye miinuko ili kujinusuru na Mafuriko hayo hasa kwa watoto wadogo ambao hawawezi kujiokoa wenyewe.
Hata hivyo Kanali Kolombo amewahimiza wakazi hao kwenda kupata huduma za kiafya katika Zahanati ya Muyuyu pindi wanapoona halli ya kiafya si shwari na kuendelea kujiandikisha kuweza kuingizwa kwenye orodha ya wahitaji.
Aidha Afisa Afya wa Wilaya Ndg. Laban Kitule yeye amewasihi wakazi hao kuhakikisha wanaweka mazingira yao safi, ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhali kwa kujenga vyoo, kuchemsha Maji ya kunywa, kula vyakula vya moto n.k ili kuweza kujikinga na magonjwa ya milipuko ambayo yanaweza kutokea.
"Tumekuja na dawa za kutibu maji ya kunywa (water guard) zitumieni kwa kufuata maelekezo ninayowapatia ili muweze kuwa na maji ya kunywa yaliyo safi na salama" Alisema Bw. Kitule.
Akitoa Salam za pole kutoka Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Afisa Mazingira Mwandamizi Ndg. Romanus Tairo amewasisitiza wananchi hao kutopuuza maelekezo yanayotolewa ili kuweza kuepuka maafa ambayo yanaweza kutokea katika kipindi hiki.
"tumekuja kubaini kiwango cha madhara yaliyotokea eneo hili, ili tuweza kuishauri Serikali hatua itakazochukua kulingana na mazingira haya kitaalam" Alisema.
Akizungumza Kwa niaba ya wananchi Ndg. Said Ally Mtakalika amewashukuru Viongozi wa Serikali kuwatembelea na kupitia ujio huo wameona ni namna gani Mama Samia anawajali wananchi wake kwani wanaamini Salam zitamfikia. Pia amesema pamoja na waathirika wa Mafuriko hayo kuandikwa majina kwa ajili ya utambuzi wa hasara walizopata, wengi bado wanahamia hivyo kuna haja ya kuendelea kuandikisha zaidi ili kupata takwimu kamili za wahanga.
Kwa upande wake Daudi Shumbi mkazi wa eneo la kifimbo amesema licha ya kuokoa mazao bado wamezingirwa na Maji, hawawezi kutoka, hivyo, wananiomba Serikali kuwasaidia usafiri boti au mitumbwi ili iweze kuwasaidia kutoka kutafuta huduma za kijamii kama vile kufuata mashine za kusaga nafaka n.k.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.