Na Cecilia Dembe, KIBITI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani inaungana na wilaya nyingine nchini kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiletea Wilaya maendeleo ndani ya miaka miwili ya uongozi wake.
Kibiti ni miongoni mwa Halmashauri za Wilaya 8 zinazounda mkoa wa Pwani, ambayo ilianzishwa Sept 2015 na kuanza kutekeleza majukumu ya kiwilaya rasmi katika mwaka fedha 2015/2016 kutoka Wilaya ya Rufiji ambapo awali ilikuwa Wilaya moja.
Katika kipindi cha miaka 2 ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumekuwa na mafanikio mengi katika Idara mbalimbali ndani ya Wilaya ya Kibiti ambayo yanatokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyoanzishwa na inayoendelea katika ngazi ya Wilaya.
IDARA YA KILIMO, MIFUGO, UVUVI NA USHIRIKA.
Uchumi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibiti kwa asilimia kubwa huchangiwa na kilimo, ambapo asilimia 78 ya pato la Halmashauri linatokana na kilimo huku mazao makuu yanayolimwa yakiwa ni Mihogo, Mahindi, Mpunga, Mtama na mazao jamii ya mikunde ambayo yanatumika kwa chakula.
Mazao ya biashara ni pamoja na korosho, ufuta, mbogamboga na Matunda na katika kipindi cha Uongozi wa awamu ya sita idara ya kilimo, Mifugo, uvuvi na Ushirika imafanya mambo mbalimbali yaliyoleta mabadiliko ya kimaendeleo.
KILIMO
Akizungumzia kuhusiana na mafanikio kwa upande wa kilimo Mkuu wa wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amesema Serikali ya Rais Samia imetoa kipaumbele kwenye Sekta ya kilimo kwa kuiongezea bajeti na kuboresha upatikanaji wa pembejeo mbolea, Viuatilifu, Mbegu bora za Korosho, Ufuta, Alizeti na vitendea kazi kwa ajili ya huduma za ugani zikiwemo Pikipiki, Vipima afya ya udongo , Vishikwambi, Bot pamoja na nyavu za uvuvi.
Kanali Kolombo amesema kutokana na vipaumbele hivyo hali ya uzalishaji wa mazao ya biashara imeongezeka na kufikia Tani 7,601,539.00 za korosho na Tani 9,060,286.00 za ufuta, wakati katika mazao ya chakula Halmashauri imezalisha Tani 39,183.50 za muhogo na Tani 23,404.30 za mpunga.
"Katika kipindi hiki cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia idara ya kilimo imepokea mgao wa pikipiki 17 kwa maafisa ugani wote wa Halimashauri hali ambayo inakwenda kurahisisha utendaji kazi kwa kuwafikia wakulima kwa wakati,"
" Pia tumepata mgao wa pembejeo za ruzuku ambapo Serikali imetoa mbolea za ruzuku takribani kg 473,928 za salfa ya unga na kuuza kwa bei ya ruzuku ya sh. 7,000 badala ya sh.15,000 na kugawanywa kwa wakulima kulingana na idadi ya miti ya mikorosho, vilevile Serikali imegawa dawa za maji lita 80,323 kwa wakulima" anaeleza Mkuu huyo wa Wilaya.
SEKTA YA MIFUGO
Akizungumzia Sekta ya Mifugo Mkuu huyo wa Wilaya ya Kibiti anasema inakadiriwa kuwa na ng’ombe 63,975, mbuzi 8,804 na kondoo 5,327.
Anaeleza kuwa mpaka sasa tayari vijiji 19 vimetenga heka 22,598.79 za maeneo ya malisho baada ya kufanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi na kwamba juhudi za kupima maeneo mengine ya malisho zinaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha.
"Katika kipindi hiki tumefanikiwa kuwa na shamba darasa moja kwa ajili ya malisho, kuimarisha barabara na kurahisisha usafirishaji wa mazao ya mifugo, pia Idara imepata zaidi ya lita 50 za dawa za kuogeshea ikiwa ni sehemu ya pembejeo za mifugo katika juhudi za kudhibiti magonjwa" anaelezaKanal Kolombo.
Amesema wamefanikiwa kupunguza idadi ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji kutoka asilimia 67 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 35 mwaka 2023 na pia wameongeza Idadi ya mifugo iliyopatiwa chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali kutoka 73,975 mwaka 2021 hadi 100,258 mwaka 2023 ambapo ng’ombe 63,975.
Wengine ni mbuzi 8,804 kondoo 5,327 ,kuku 18,0041 na mbwa 1,600, na kwamba wameongeza uzalishaji wa nyama na maziwa kutoka tani 40,523 mwaka 2021 hadi kufikia tani 90,720 kwa mwaka 2023.
UVUVI
Kanali Kolombo amesema miongoni mwa mambo muhimu yaliyotekelezwa na kufanikiwa Kwa mwaka wa fedha 2021/22 na 2022/23 katika sekta ya Uvuvi ni pamoja na kuongezeka kwa mabwawa ya wafugaji wa samaki kutoka wafugaji wanne hadi kufikia 15, na doria zimeongezwa kufanyika kwa ajili ya kukabiliana na uvuvi haramu kutoka doria 24 hadi 30 na kuongezeka kwa uzalishaji wa samaki kutoka tani 571.3 hadi kufikia Tani 731.5 sambamba na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na samaki kutoka sh. Milion 105 hadi sh.Miln 147.
Mkuu huyo wa Wilaya anaendelea kueleza kuwa katika Wilaya hiyo Shughuli za uvuvi hufanyika maeneo ya mito iliyopo delta (visiwani) yenye urefu wa km 75 kutoka kusini hadi kaskazini na eneo la bahari kuu ambapo km 700 za eneo hilo linaingia ndani ya ardhi.
Kanal Kolombo anasema sekta ya uvuvi katika Wilaya ya Kibiti imewezesha watu 4,136 kwa kujiajiri wenyewe ambapo watu 3,729 hufanya ajira ya kudumu na watu 407 ni kwa ajili ya chakula.
kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya Sekta ya uvuvi inachangia upatikanaji wa chakula kipato na kuinua uchumi kwa jamii, wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla.
KITENGO CHA USHIRIKA
Kwa miaka miwili ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suhusu Hassan Wilaya kibiti tumefanikiwa kuongeza Idadi ya vyama vya Ushirika kutoka 16 hadi 22, kuongeza kiasi cha mazao yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa asilimia 87.75 kuongezeka kwa hisa za wanachama kwa asilimia 34.
Kwa upande wa vyama vya ushirika Wilaya ina vyama 22 vinavyojumuisha vyama vya mazao (AMCOS) 21, na chama kimoja cha Akiba na Mikopo yaani (SACCOS).
Vyama hivyo vina wanachama 1,849 na SACCOS zenye mtaji wa sh. 257,372,227 inayojumuisha Hisa, Akiba na Amana. Aidha mikopo yenye thamani ya sh. 97,286,250 imetolewa kwa wanachama.
IDARA YA AFYA
UIMARISHAJI WA SEKTA YA AFYA.
Mkuu wa Wilaya amesema Wilaya amesema ni kati ya maeneo yaliyonufaika kimaendeleo katika kipindi cha miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita kwenye Sekta ya afya, ambapo Serikali imeendelea kutoa fedha za kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambayo kwa sasa imeanza kutumika.
Hata hivyo katika kuimarisha na kuboresha sekta ya Afya, Wilaya imepata Vituo vya afya 5, viwili ambavyo viko katika hatua za ukamilishaji na tayari vimeanza kutoa huduma za dharura katika maeneo kivinja “A” HC , Mjawa HV.
Katika miaka miwili ya Rais Samia vituo viwili vya afya vya Mbwera na Kibiti vimeboreshwa na kwa sasa hutoa huduma za kisasa zaidi na za dharura wakati huo huo ujenzi wa kituo kipya cha afya cha Nyamatanga ukiendelea.
" Tmefanikiwa pia kupata Zahanati 10 ambapo kati ya hizo 6 zimekamilika na kuanza kutoa huduma, na kati ya Zahanati nne zilizosalia mbili zinatarajiwa kukamilika na kuanza kutoa huduma mpaka kufikia Mei 2023 nyingine mbili ujenzi wake ukiendelea" anaeleza Kanal Kolombo.
Amesema pamoja na fedha nyingi zilizotolewa na Serikali Kwenda kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo pia Wilaya imepokea sh Miln 800 kwa ajili ya ujenzi wa majengo manne (Jengo la upasuaji, Jengo la kuhifadhia maiti, na majengo mawili ya upasuaji kwa ajili ya wanawake na wanaume) ambayo yapo katika hatua za umaliziaji na kufanya Hospitali kuwa na jumla ya majengo 15.
Hospitali hiyo inauwezo wa kuhudumia wakazi wa kibiti na maeneo ya Wilaya za jirani sambamba na pia ina wataalam nguli katika vitengo mbalimbali Pamoja na vifaa tiba vya kisasa, hivyo kutokana na upatikanaji wa vifaa tiba hivyo hospitali imeweza kutoa huduma kwa wakazi wake.
Huduma zinazotolewa ni kwa wagonjwa wa nje,magonjwa yasiyoambukiza na yanayoambukiza, macho, kinywa na meno, unasihi na upimaji wa maambukizi ya VVU, huduma ya magonjwa ya wanawake na wanaume na upasuaji, kliniki ya baba, mama na mtoto, bima ya Afya, magonjwa ya dharura na sasa Hospitali imeanza kutoa huduma ya mionzi ambampo tayari mashine ya ultra sound inayotoa huduma kwa wagonjwa wote, X- ray hii ni ya kisasa yenye thamani ya sh miln 460 yaani Digital X-Ray mashine.
Pia limejengwa jengo la kuhudumia wagonjwa wa dharura (EMD) lenye thamani ya sh 300,000,000 ambalo limefungwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa dharura.
ELIMU.
Katika idara ya Elimu chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan,kwa upande wa shule za sekondari Wilaya ya kibiti Imenufaika kwa kujengewa shule mpya tatu za Sekondari, vyumba 85 vya madarasa, katika kurahisisha kazi idara imepokea na kugawa vishikwambi 278 kwa Walimu wote na magari mawili kwa ajili ya elimu sekondari na msingi.
Pia katika idara ya Elimu kwa upande wa shule za msingi Wilaya imefanikiwa kupata vyumba 38 vya madarasa, matundu 73 ya vyoo na ujenzi wa nyumba nne za walimu , ujenzi wa Bweni la Watoto wenye mahitaji maalumu, vilevile maboma tisa ya vyumba vya madarasa yaliyoanza kwa nguvu za wananchi yamekamilishwa katika kipindi hiki cha awamu ya sita, mbali na hayo walimu wa shule za msingi wamepatiwa jumla ya vishikwambi 634.
NYUMBA ZA VIONGOZI NA WATUMISHI
"Ndani ya kipindi cha miaka miwili ya mama Samia madarakani tumefanikiwa katika ujenzi ya nyumba za watumishi zenye ubora wa hali ya juu kwa ajili ya viongozi na watumishi wa kada mbalimbali, kwa kukamilisha ujenzi wa nyumba moja ya Katibu Tawala wa Wilaya , Mkurugrnzi wa Halmashauri na nyumba nne za walimu bado zinaendelea na ujenzi, nyumba vitatu za watumishi wa afya na
AJIRA MPYA.
Rais Samia katika utawala wake ametoa ajira katika baadhi ya Idara ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imenufaika kwa kupokea rasilimali watu yenye jumla ya watumishi 172 wa ajira mpya katika idara mbalimbali, ambao wanakwenda kuongeza nguvu kazi ya utendaji wenye tija wilayani Kibiti
MIKOPO YA WANAWAKE, VIJANA NA WALEMAVU.
Serikali katika kuhakikisha inakuza na kutoa fursa za Ajira nchini kupitia makato ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti chini ya Idara ya maendeleo ya jamii, Imefanikiwa kuunda vikundi na kutoa mikopo kwa wanawake, vijana na walemavu mbalimbali ambapo tayari sh miln 515 zimekopeshwa kwa wanawake, vijana na mlemavu hali iliyowajengea uwezo kujikwamua kiuchumi kwa kujiajiri na kujiingizia kipato ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
MIUNDOMBINU
Tarura-barabara.
Wakala wa barabara za Vijijini na mijini wilaya ya kibiti kwa kipindi cha Julai 2022 mpaka Feb 2023 kimetengewa kiasi cha sh 2,657,720.00 kutoka mfuko wa barabara (road fund).
Anaeleza kuwa Kupitia fedha hizo matengenezo mbalimbali ya barabara, madaraja na makalavati yamefanyika na kazi hizo bado zinaendelea kwa urefu wa km 171.53 kwa fedha za matengenezo, km 0.6 kwa fedha za maendeleo ya Jimbo, km 28 kwa fedha za maendeleo ya tozo na km 7 kwa fedha za mfuko wa barabara.
Katika taswira hiyo kwa upande wa miundombinu ya barabara tayari Serikali imeweka fedha za kutosha kuwawezesha Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuendeleza miundombinu ya barabara mpaka vijijini.
UMEME.
Kanal Kolombo ameelezea kuwa katika Nishati ya umeme, Shirika la umeme TANESCO Wilaya ya Kibiti limetengewa sh. 406,695,954.44 kwa ajili kuhakikisha inasambaza umeme ndani ya wilaya na tayari upembuzi yakinifu umekwisha fanyika kwa asilimia 100 katika maeneo mbalimbali ndani ya wilaya na kazi zinaendelea.
REA
Inaelezwa kuwa miaka miwili ya utawala wa Serikali ya awamu ya sita Wakala wa Umeme vijijini REA wamefanikiwa kupokea sh.5,504,402,215.71 za miradi ya ujazilizi ambapo tayari wamekwisha kuwaunganishia umeme wateja 186 lengo likiwa ni kuwafikia wakazi 1,028 kwa usimamizi wa mkandarasi SENGEREMA ENGINEERING GROUP LTD.
Vilevile katika awamu ya tatu mzunguko wa pili ya mradi wa REA sh.37,798,369,028.21 zimepokelewa na katika awamu hiyo na wateja wanaotakiwa kuunganishiwa umeme ni 206 tayari wateja 160 wameshaunganishiwa umeme sawa na asilimia 77.7 ya wateja ambao hawajaunganishiwa na shughuli hizo zinatekelezwa na Mkandarasi CHINA RAILWAY CONSTRUCTION ELECTICTICATION BUREAU GROUP CO.LTD (CRCEBG).
MAJI
Kwa upande wa maji anasema miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, Wilaya imenufaika na miradi 13 ya maji, iliyopo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ofisi na nyumba za watumishi yenye thamani ya sh. 8,757,976,431.86.
Anasema Baada ya Kukamilika kwa miradi hiyo inatarajiwa kuwafikia wakazi 48,347 hivyo itarahisisha upatikanaji wa maji Safi, salama na ya uhakika ndani ya Wilaya ya kibiti.
Amesema miradi hiyo ipo katika Vijiji vya Kilulatambwe, Mjawa, Mtunda , Nyanjati – Kivinja A, Kikale, Bumba, Msoro, Mlanzi, Jaribu Mpakani, Mtawanya, Uponda, Mchukwi, Mkenda/Kivinja B yote ikitekelezwa kwa fedha za NWS wakati mradi wa maji Mahege ukijengwa kwa fedha za (Uviko 19).
WAKALA WA MISITU (TFS)
Kanal Kolombo amesema kwa upande wa misitu katika kipindi cha miaka 2 ya Uongozi wa Rais Samia Wilaya imefanikiwa kulinda misitu isiharibiwe kwa kuimarisha na kufanya doria za mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kuweka mawe ya alama ili kuijulisha Jamii mipaka ya misitu hiyo
Pia katika kipindi hiki TFS kwa ushirikiano wa serikali na wadau mbalimbali katika wamerejesha uoto wa asili Mwambao wa Pwani, ambapo wamepanda miche 2,026,451 kwenye hekari 201.55 ya miti ya mikoko ndani ya hifadhi ya delta ya Rifiji,Taasisi za umma,Taasisi za dini na mashamba ya watu binafsi.
Mwisho
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.