Tatizo la Mimba za utoroni sambamba na utoro mashuleni limeendelea kuwa kikwazo katika Wilaya ya Kibiti jambo linalofanya watoto kushindwa kumaliza shule na kutimiza ndoto zao.
Hayo yamejiri katika kikao cha tathmini ya mimba mashuleni kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri tarehe 12.2.2024, majira ya mchana.
Katika kikao hicho Mkuu wa wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amesema kutokana na ugumu unaojitokeza kuwataja wanaowatia mimba wanafunzi, Sasa ataanza kukamata wazazi wa watoto waliopata ujauzito hususani kinamama kwa sababu wamekuwa wakijua kinachoendelea na kuficha siri.
"Nitapambana na wazazi , kinamama wamekuwa wanawafichia siri watoto wao, nitawakamata wote" Alisema Kanali Kolombo.
Hivyo Halmashauri imeweka mikakati ya kuondoa tatizo la mimba ikiwemo usimamizi thabiti wa upimaji mimba mashuleni ambao pamoja na Wahudumu wa Afya pia utasimamiwa na Watendaji Kata, Maafisa Elimu Kata, Polisi kata, walimu Wakuu na Wakuu wa shule.
Maazimio mengine ni kuhakikisha elimu ya mimba inatolewa mashuleni kupitia Watendaji Kata, Polisi kata, Ustawi wa jamii, Maendeleo ya jamii, dawati la jinsia na Maafisa Elimu Kata.
Pia Polisi kata wote wameagizwa kupeleka taarifa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hususani Orodha ya kesi za mimba zilizofikishwa Polisi na mahakamani.
Mwisho Mkurugenzi Mtendaji Hemed Magaro amewaagiza watendaji Kata wote kupeleka taarifa ya watoto walioripoti shuleni kuanzia wale wa darasa la Awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.