tarehe 14.6.2023 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa idara zote wa Wilaya ya Kibiti, ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipowasili kituo chake kipya cha kazi akitokea Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora.
Akiwa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri Mkurugenzi Magaro amemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini katika kumsaidia majukumu ya kuwatumikia na kuwaletea maendeleo watanzania.
Mara baada ya utambulisho, Magaro amewataka Watumishi wote kila mmoja kulingana na majukumu yake kufanya kazi kwa weledi na kujituma, kama kanuni na taratibu za kazi zinavyoelekeza.
Vilevile Magaro amesema ili kazi ziende anahitaji ushirikiano wa kutosha kwa watumishi wote, ili kuweza kuwa na Maendeleo chanya katika Wilaya ya Kibiti.
" Ninaomba ushirikiano wenu, bila ninyi peke yangu sitaweza hivyo tushirikiane tuchape kazi, na kwenye kazi napenda matokeo ya haraka"Alisema Magaro.
Aidha kwa niaba ya watumishi wote wa Wilaya ya Kibiti Afisa Elimu Sekondari Mwl. Anna Shitindi akimkaribisha Mkurugenzi Magaro alisema kuwa, watumishi wote wapo tayari kumpa ushirikiano na kupokea maelekezo yake ya kazi.
Awali Afisa Utumishi Msena Bina akimtambulisha rasmi Mkurugenzi huyo mpya kwa watumishi, alimpongeza kwa kuendelea kuaminiwa kuwatumikia watanzania. Hata hivyo Msena Bina aliwatambulisha watumishi Pamoja na wakuu wa idara na vitengo kwa Mkurugenzi.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.