Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro ameyataka Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayofanya kazi Wilayani Kibiti kutokufanya kazi kiholela, ameyataka mashirika hayo kujulikana kisheria na kufuata miongozo ya ufanyaji shughuli za kiasasi ndani ya Halmashauri.
Ndg. Magaro amesema hayo leo Agosti 21, 2024 alipokuwa akifungua kikao cha Jukwaa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali Wilayani Kibiti kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, ambapo mashirika 21 yalialikwa.
“Serikali inatambua ukubwa wa mchango wenu kwenye jamii, bila nyie kuna mambo ambayo yasingeweza kutekelezwa na Serikali pekee. Hivyo basi niwaombe mkifika njooni kwenye uongozi mjitambulishe na shughuli mnazokwenda kufanya ili mpate kibali lakini pia tambulisheni kwanza kila mradi mnaotaka kuutekeleza kwa uongozi wa wilaya, kata na vijiji kabla ya kuwafikia Wananchi, msiende moja kwa moja kwao” Alisema.
Mkurugenzi huyo ameyataka mashirika hayo kutoa Elimu inayozingatia tamaduni zetu za Kitanzania, pia kutoa elimu ya mpiga kura kwa jamii hususani wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kwani ari ya watu kushiriki shughuli za uchaguzi wa viongozi bado ipo chini haswa kwa vijana.
Vilevile Ndg. Magaro ametumia jukwaa hilo kuyakumbusha mashirika hayo kuwasilisha taarifa za utendaji kazi wao kwa kila robo ya mwaka ambao watabainisha miradi na kiasi cha fedha kilichotumika kutekeleza miradi hiyo ili kuonesha uwazi kwa jamii.
Mwisho kabisa Mkurugenzi Magaro ameahidi kutoa ushirikiano kwa mashirika hayo huku akiwaomba wawaalike wengine kwani Kibiti bado ina uhitaji wa wadau wengi zaidi watakaoweza kusaidia miundo mbinu ya Elimu na Afya.
Aidha Halmashauri imeyamezawadiwa vyeti Mashirika 3 kwa kutambua mchango wao katika kusaidia jamii ya Kibiti. Mashirika hayo ni Jicho Angavu, Kalamu Education Foundation pamoja na CAMFED.
Kwa upande wao wawakilishili wa mashirika hayo wameishukuru Halmashauri kwa kuwapa ushirikiano na kutoa maombi ya kupatiwa Mkaguzi wa hesabu kila mwisho wa mwaka ili watoe taarifa sahihi, kupewa Ofisi pale jengo la Halmashauri litakapokamilika pamoja na ushiriki wa wataalam kama Mwanasheria, Afisa maendeleo ya jamii, Afisa Elimu na Afisa biashara kwenye vikao vyao kwani shughuli nyingi zinagusa sekta hizo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.