MKUU WA WILAYA YA KIBITI ATEMBELEA NA KUKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA MAEGESHO YA DARAJA LA MBUCHI LENYE UREFU WA MITA 61.
Leo tarehe 27.07.2021Mheshimiwa mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali.Ahmed Abasi Ahmed ametembelea na kufanya ukaguzi wa ujenzi wa maegesho ya daraja la Mbuchi lenye urefu wa mita 61, ambapo aliongozana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya,Mkurugenzi Mtendaji na baadhi ya watendaji wa Halmashauri, meneja wa RUWASA pamoja na Mhandisi wa TARURA.
Mradi huu unasimamiwa na wakala wa barabara vijijini(TARURA) na kujengwa na kampuni ya Alpha Logistics ya Tanzania utagharimu kiasi cha shilingi 6,145,882,290.38 ambapo utajumuisha ujenzi wa maegesho mawili(abutments),barabara za mkaribio za daraja mita 200 kila upande,maboresho ya barabara kutoka Muhoro kwenda Mbuchi kilometa 23 pamoja na kuimarisha daraja la Muhoro.
Mradi huu ulianza tarehe 04.01.2021 na unatarajiwa kukamilika Desemba,2021 mpaka sasa mradi huu umetekelezwa kwa asilimia 57.
Baada ya ukaguzi Mhe.mkuu wa Wilaya Kanali.Ahmed A. Ahmed aliridhishwa na maendeleo ya ujenzi na kumtaka mkandarasi aongeze kasi ili mradi huu ukamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi kwani serikali ina jukumu la kuleta maendeleo kwa wananchi wake na daraja hili linaenda kutatua kero ya muda mrefu kwa kuunganisha vijiji vya kata hii.
Diwani wa Kata ya Mbuchi Mhe.Yusuf Saidi Mpili kwa niaba ya Wananchi alishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha ya kujenga daraja hili ambalo lilikuwa kero kubwa kwa wananchi wa kata ya Mbuchi kwa muda mrefu pia Mheshimiwa Diwani aliomba Serikali kuona umuhimu wa kuongeza mita nyingine zaidi za matengenezo ya barabara ya mkaribio wa daraja kwa upande wa kuelekea vijiji vya Mbwera Magharibi na Mashariki kwani bila kufanya hivyo daraja hili litakuwa halifanyi kazi iliyokusudiwa.Mhandisi wa wakala wa barabara vijijini(TARURA) Eng.Salim Bwaya ambaye ndie msimamizi mkuu alisema suala hilo walishaliona na wiki ijayo atatuma wataalam kutoka ofisini kwake kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina ili kupata mahitaji na kazi hiyo itatekelezwa ili daraja hilo lifanye kazi iliyokusudiwa.
Aidha, baada ya ukaguzi huo Mheshimiwa mkuu wa wilaya alifanya kikao na Wananchi wa Mbuchi kwa lengo la kujitambulisha na kusikiliza kero zao na kuahidi kuzifanyia kazi.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.