MNADA WA KWANZA WA KOROSHO KIMKOA WAFANYIKA WILAYANI KIBITI
Posted on: November 2nd, 2022
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Meja Edward Gowele kwa niaba ya Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameongoza uzinduzi wa mnada wa kwanza wa mauzo ya korosho Mkoa wa Pwani uliofanyika katika Wilaya ya Kibiti.
Katika mnada huo jumla ya kilo 1,713,462 zimeuzwa, daraja la kwanza likiwa na kilo 1,658,990 ambazo zimeuzwa kwa bei ya wastani ya shilingi 1,661.94 na daraja la pili likiwa na Kilo 54,472 ambazo zimeuzwa kwa bei ya shilingi 1,405 baada ya Wakulima wote kukubaliana kuuza kwa Bei zilizoainishwa.
Awali Meneja wa Corecu Mkoa wa Pwani Hamisi Mantaleo alisoma zabuni za wanunuzi 11 ambazo ziliwasilishwa kwa njia ya sanduku. Na mnada ujao utafanyika tarehe 9/11/2022 Wilayani Mkuranga.
Vilevile Mantaleo amewataka wakulima na wanunuzi kujenga tabia ya kusoma na kuelewa vizuri makato ya tozo kama yanavyoainishwa kwenye makabrasha kabla ya mnada ili kuepusha sintofahamu kuhusu makato hayo ambapo jumla ya tozo za taifa ni 206.94, kwa Mkoa wa Pwani makato ni sh 20 kwa ajili ya kuchangia Elimu, na sh 20-81 kwa ajili ya usafiri kutoka kwenye magala ya AMCOS mpaka gala kuu (Inategemeana na umbali).
Hata hivyo Meja Gowele ameahidi kubeba na kufanmyia kazi suala la makato makubwa ya korosho (tozo) hususani bei za kuuza korosho zinapo kuwa chini kama ilivyo mwaka huu, kwani Serikali ni sikivu na ipo kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi wake .
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Mauzo Mkoa wa Pwani Bi Domina Adman akijibu swali lililoulizwa na mkulima kuhusu tozo amesema Tozo ya Tali Naliendele ambayo ni sh. 25 kwa kilo haijafutwa ipo kwa lengo la kusaidia kuendeleza tafiti mbalimbali kuanzia ngazi ya uzalishaji mpaka usindikaji.