Wakulima wa korosho Mkoa wa Pwani wameingiwa na hofu ya ubora wa korosho kushuka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini na kusababisha zoezi la ukaushaji wa bidhaa hiyo kuwa mgumu.
Hayo yamesemwa Jumatano, novemba 15 katika mnada wa pili uliofanyika Wilayani Mkuranga ambapo jumla ya kg 14,189.23 zimeuzwa, daraja la kwanza zikiuzwa kwa bei ya wastani ya sh 1809 .89 na daraja la pili kuuzwa kwa bei ya wastani wa sh 1300 baada ya wakulima wote kukubaliana kwa pamoja baada ya kuchakata na kupata bei ya wastani wa juu na chini kulingana bei zilizowasilishwa na wazabuni 10 kwa njia ya sanduku.
Kutokana na hali hiyo, upokeaji wa mzigo kwenye maghala umekuwa mdogo kwasababu kwa kawaida korosho yenye ubora inayotakiwa ni ile iliyokauka vizuri ukilingamisha na msimu huu korosho nyingi zina unyevu..
"Unyevu wa korosho unatakiwa usizidi asilimia 10 lakini kwa kipindi hiki haukwepeki" walisema wakulima hao kwa nyakati tofauti.
Aidha Wakulima hao waliendelea kudai kuwa katika msimu huu mavuno ni mengi lakini wanatarajia kuwa na hasara kubwa kutokana na mvua zinazonyesha kwani kutokauka vizuri kwa korosho hizo moja kwa moja kunakosesha sifa ya kupata masoko na bei kushuka kwa ujumla.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.