.
21.5.2023
Mwenge wa uhuru 2023 umeridhia miradi 15 ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti yenye jumla ya sh.Bil 1.3 kwa kuikagua, kuzindua, kufungua sambamba na uwekaji wa mawe ya msingi baada ya kujiridhisha na kutoa maelekezo mbalimbali kwa kuchagizwa na Kauli mbiu yenye usemi usemao Tunza Mazingira Okoa Vyanzo vya Maji, kwa Ustawi wa Viumbe hai kwa Uchumi wa Taifa.
"Tumepokea taarifa ya miradi, tumekagua na kuridhishwa na miradi yote pamoja na nyaraka zote", Alisema Kaim.
Hayo yamebainishwa na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Taifa 2023 Ndg. Abdallah Shaib Kaim baada ya Mwenge wa Uhuru kumulika na kuridhia miradi hiyo.
Mkimbiza Mwenge Taifa Ndg. Abdallah Shaib Kaim ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kwa kusimamia vizuri miradi ya Maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali na mapato ya ndani huku akimshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo Wilayani Kibiti na Nchi nzima Kwa ujumla.
"Nichukue fursa hii kuwapongeza Viongozi wote wa kibiti kutokana na utendaji wenu na itoshe kusema kwamba, Mwenge wa Uhuru, unatambua mchango wenu mkubwa katika kupigania maendeleo ya Wilaya hii." Alisema Abdallah Shaib Kaim.
Aidha Kaim ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kutafuta vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitasaidia kuongeza ukuaji wa pato la wilaya na kuendelea kujiletea maendeleo.
Akikagua mradi wa ujenzi wa nyumba ya wageni Top 5 amewataka wakazi wa kibiti kujifunza kupitia Mwekezaji huyo alimaarufu kwa jina la mjomba Dani kuwekeza ndani ya Wilaya jambo linaloonyesha Uzalendo Mkubwa na litakalosaidia kukuza pato la wilaya.
Akisoma Salam za Mwenge wa Uhuru ndg. Kaim amewataka wananchi kuhakikisha wanahifadhi mazingira hususani katika vyanzo vya maji ili kuweza kuendana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa ni tatizo kubwa Duniani kote.
Hata hivyo katika salamu hizo za Mwenge ndg Kaim amesisitiza wananchi kuhakikisha wanapambana na adui wa Maendeleo (Rushwa) kwa kuepuka kushiriki aina yoyote ya rushwa na Kwa kutoa taarifa za viashiria vya rushwa na ushahidi mahakamani ili kufanikiwa kudhibiti changamoto hiyo. Licha ya Salamu hizo pia amewataka wananchi kukabiliana na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya kwa kuepuka kujishughulisha na uuzaji na uzalishaji wa dawa hizo Pamoja kuendelea kuwaelimisha walioathiriwa na dawa hizo kutorudia tena kutumia dawa hizo.
Hakuishia hapo katika salamu za Mwenge amewasihi wananchi kupambana na mapambano dhidi ya Malaria yenye kauli MBIU isemayo, "zero malaria inaanza na Mimi, chukua hatua kuitokomeza"
Bila kusahau ulaji wa lishe bora yaani mlo kamili, kwani lishe Bora hujenga afya imara na kuleta maendeleo ya afya imara kwa watu wote, hususani katika makundi 5 ya vyakula ambayo ni ulaji wa mbogamboga kwa wingi, mafuta, nafaka kidogo, matunda na sukari.
Mbali ya salamu hizo vilevile amewasisitiza wananchi wa kibiti kukabiliana na mapambano ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kuimarisha USAWA, kutokomeza ukatili wa kijinsia, kuhudhuria vituo vya afya kupima afya na kuanza kutumia dawa za kufubaza endapo mtu atagundulika ameathirika
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.