Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Ndeliananga amezindua nyaraka za usimamizi wa maafa Wilaya ya Kibiti siku ya Jumanne 23.7.2024 huku akisisistiza nyaraka hizo kutekelezwa kwa vitendo.
Mhe. Ndeliananga amesema uzinduzi huo ni mwanzo wa kuanza kazi rasmi endapo kutatokea janga lolote, na kutoa wito kwa idara, vitengo na taasisi ngazi ya Wilaya kuzingatia dira hiyo katika kutekeleza vipaumbele vya kisekta.
Vilevile Naibu Waziri huyo amesema tathmini ya maafa iliyofanyika katika Wilaya ya Kibiti mwezi Juni 2024 imeonyesha kuwa Wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na maafa yanayosababishwa na majanga makubwa ya upepo mkali na mafuriko na hivyo basi matokeo ya tathmini hiyo yamezingatiwa katika kuandaa mpango wa kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali baada ya maafa.
Mbali na hayo pia amesema nyaraka hizo zikawe chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau kwa kuwajengea uwezo juu ya masuala ya Maafa ikiwa ni pamoja na kuimarisha mfumo wa utoaji wa taarifa za tahadhari za awali sambamba na kuzingatia namna ya kuwawezesha walemavu wa aina mbalimbali kupata taarifa za nyaraka kulingana na uhitaji wao.
Hata hivyo Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Brigedia Generali HOSEA NDAGARA amesema Idara hiyo imekuwa ikichukua hatua za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa na kurejesha hali ambapo shughuli mbalimbali zimekuwa zikitekelezwa ikiwemo kuratibu upatikanaji wa vifaa.
Kwa upande wake Mtaalam wa Mradi wa UNDP ambao ndiyo wadhamini ya mafunzo na utengenezwaji wa nyaraka hizo Ndg. Abbas Kitogo amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika masuala ya majanga na maafa huku akisema ni wakati wa wadau wengine sasa kujitokeza kuongeza nguvu ili kuweza kuzifikia Wilaya zingine nchini lengo likiwa ni kutoa uelewa kwenye jamii.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu na UNDP kwa kuwawezesha kupata mafunzo na mwongozo kwani utawasaidia sana endapo watapatwa na maafa. Pia kupitia mafunzo na miongozo waliyopatiwa ameahidi kuhakikisha inafanyiwa kazi, kuendelea kuipitia mara kwa mara na kuifikisha kwenye jamii.
Mara baada ya kukabidhiwa nyaraka hizo zilizozinduliwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro amesema, wanashukuru kwa kupata nyenzo hizo za kufanyia kazi na atahakikisha kuwa mpango huo unaingia katika bajeti ya Halmashauri ikiwa ni sehemu ya kujiimarisha kumudu kujiwezesha pindi maafa yakitokea.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kibiti Bw.Maliki Magimba akitoa Salam za Chama amesisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhali za maafa kwa kukaa mbali na maneno yenye historia ya kuwa na majanga hayo mara kwa mara.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.