Jana Agosti 29, 2024 Benki ya NMB imekabidhi Madawati 120 kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti ikiwa ni sehemu ya kurudisha shukrani kwa Jamii ya Kibiti kwa kuendelea kuiamini na kutumia benki hiyo. Msaada huo ni matokeo ya Ombi la Mh. Mkuu wa Wilaya Kibiti Kanali Joseph Kolombo alilotoa mapema mwezi Januari mwaka huu katika kikao chake na Wadau wa Elimu.
Kanali Kolombo aliwaomba Wadau hao kusaidia miundo mbinu katika Sekta ya Elimu hususani Meza na Viti kwa Shule za Sekondari pamoja na Madawati kwa Shule za Msingi, kwani Wanafunzi wengi bado wanakaa chini. Hivyo basi NMB wamefanikisha Jambo hilo kwa kuchangia madawati 120 yenye thamani ya Sh. Milioni 12.
Akikabidhi Madawati hayo Meneja wa NMB Kanda ya Dar-es-Salaam na Pwani Bw. Seka Urio amesema, NMB imefarijika sana ilipopokea maombi ya kuchangia madawati ili kuboresha mazingira ya kusomea kwa Wanafunzi na kuona imeheshimika kushiriki kuunga Mkono jitihada za Mhe. Rais katika kuboresha miundo mbinu ya Elimu nchini.
“Kibiti tuna Wateja wengi sana kama vile Walimu, Wafanyabiashara na Wananchi, hivyo kile ambacho NMB inakipata kwa kufanya biashara na jamii hiyo, baada ya kulipa kodi ya Serikali huwa tunatenga 1% ya faida na kurudisha kwa jamii tunayofanya nayo kazi huku kipaumbele chetu siku zote kikiwa ni Elimu, Afya na wale wanaopata changamoto ya Majanga. Kwahiyo madawati haya ni sehemu ya fedha hizo”. Alisema Bw. Urio
Aidha Kanali Kolombo ameishukuru sana benki hiyo kwa Madawati na misaada mingine iliyowahi kutolewa hapo awali kama vile Bati 120 zilizotolewa mwezi Januari mwaka huu ambazo zilisaidia kupaua nyumba za walimu waliokuwa hawana pa kukaa.
“Tunawashukuru sana NMB kwa misaada mingi mnayoendelea kutuletea Kibiti maana si Madawati haya tu yapo yale ya 2018 ambayo tumepita huko darasani na kuona yametunzwa vyema na bado yapo imara. Lakini pia nakumbuka mlituletea bati 120 ambazo zilisaidia kupaua nyumba za Walimu, Sasa naona ipo haja ya nyie kutenga siku 1 mje kututembelea ili muone misaada mliyotoa inaendeleaje, Sisi Kibiti tunaahidi kuitumia kama ilivyokusudiwa” Alisema Kanali Kolombo.
Akitoa salamu za chama Katibu wa CCM Wilaya ya Kibiti Ndg. Malik Magimba ameishukuru sana benki ya NMB kwa moyo wao wa ukarimu na jitihada zao za kuiunga mkono Serikali katika sekta ya Elimu huku akiwasisitiza kutokusita kuendelea kutoa misaada pale watakapoombwa tena kwani chanamoto bado ni nyingi kwa Wilaya ya Kibiti.
Naye Mwenyekiti wa Hamashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Ramadhani Mpendu kwa niaba ya baraza la Wahe. Madiwani ameishukuru sana benki hiyo kwa kuwa msaada huo waliotoa utapunguza adha ya madawati katika kata 5 kati ya 16 za Hamashauri ya Wilaya ya Kibiti.
Mwisho kabisa Halmashauri imetoa cheti cha pongezi kwa NMB kwa kutambua mchango wao katika Sekta ya Elimu.
Madawati hayo yamegawanywa katika shule 5 kama ifuatavyo: Madawati 40 Shule ya Msingi Kitundu, Madawati 25 Shule ya Msingi Jaribu Mpakani, Madawati 25 Shule ya Msingi Mkwandara, Madawati 20 Shule ya Msingi Maparoni na Madawati 10 Shule ya Msingi Kinyanya.
Wote kwa pamoja, Walimu na Wanafunzi waliopokea madawati hayo wameahidi kuyatunza vyema.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.