Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Mgeni rasmi wa siku ya tarehe 04.08 2024 Mhe. Alexander Mnyeti ametoa wito kwa Taasisi za UMMA kupeleka bidhaa zenye ubora zaidi kwenye Maonesho ili Sekta binafsi zikapate kujifunza na kutambua nini Serikali inafanya.
Mhe. Mnyeti Amesema hayo kwenye Maonesho ya 88 yanayoendelea katika Viwanja vya Mwl. J.K Nyerere Manispaa ya Morogoro alipotembelea mabanda mbalimbali.
Vilevile Naibu Waziri huyo ametoa wito kwa Wananchi kujitokeza kutembelea Maonesho ya nanenane ili waweze kujifunza kwa kuona wenyewe ni nini kinafanyika.
"Wito wangu kwa wananchi, 88 ni darasa tosha, nendeni mkatembelee mjifunze nini kinafanyika huko" Alisema.
Mara baada ya kukagua mabanda hayo amewapongeza Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Idara na Vitengo, Watumishi mbalimbali pamoja na Sekta binafsi kwa namna wanavyotumia nguvu kubwa kuhakikisha wanaibadilisha nchi kwani ni ishara tosha kuwa, kuna elimu inatolewa katika maeneo yao kulingana na vitu vinavyooneshwa.
"Leo nimejifunza kwa ukubwa wa pekee namna teknolojia inavyotumika kuleta mabadiliko chanya kwenye Sekta ya Kilimo Mifugo na Uvuvi sambamba na Uwekezaji" Alisema.
Aidha kipekee amezipongeza Sekta binafsi kwa uzalendo wanaouonyesha kwani licha kufanya biashara wanatoa huduma na kuwekeza kwa kuzalisha bidhaa tofauti kwa kutumia viwanda vya ndani.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.