8.5.2024.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila Mwenge wa Uhuru baada ya kukimbizwa katika Mkoa wa Pwani kwa takribani siku 9 ndani ya Wilaya 7 zenye jumla ya Halmashauri 9.
Akisoma taarifa ya Mkoa wa Pwani wakati akikabidhi Mwenge wa uhuru Mhe. kunenge amesema Mwenge umekimbizwa km 1,225.3 katika Wilaya zote za Mkoa huo na kumulika jumla ya miradi 126 yenye thamani ya sh Trillion 8.536 ambapo miradi 18 imekakaguliwa, 22 imezinduliwa na 86 imewekewa mawe ya Msingi.
Kunenge amebainisha kuwa kati ya miradi 126 iliyomulikwa miradi 2 imeonekana kuwa na dosari ambayo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa ametoa maelekezo, na kuahidi kwamba dosari hizo zinakwenda kufanyiwa marekebisho ndani ya muda mfupi kwa kufuata maelekezo waliyopewa.
"Tumepokea maelekezo na tunakwenda kuyafanyia kazi ndani ya muda mfupi kwa tulivyoelekezwa" Alisema Kunenge.
Kwa nyakati tofauti viongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 wakiongozwa na Kiongozi wa Mbio hizo Kitaifa Ndg. Godfrey Eliakimu Mzava wameupongeza Mkoa wa Pwani kwa mashirikiano mazuri na utayari wao waliouonyesha tangu walipoingia mkoani humo ikiwa ni pamoja na wananchi, Vyombo vya Usalama, Wakuu wa Wilaya ,Vijana wa halaiki, jukwaa la wazalendo huru n.k.
"Tunatamani tuendelee kuwepo Pwani lakini inatupasa kuelekea Dar es salaam kwa mujibu wa ratiba, tangu tumeingia Mkoa wa Pwani hatujakutana na changamoto yeyote na Mwenge unaondoka ukiwa salama" Alisema Mzava.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.