Serikali ya Tanzania ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza kupitia mfuko wa UK Aid imetoa semina kwa waandishi wa habari mkoa wa Pwani juu mradi kabambe wa shule bora nchini , kwa dhumuni la kuboresha elimu na kumfanya mtoto kupata msingi mzuri kuanzia ngazi za awali.
Katika mkutano huo Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Zuwena Omari amesema Serikali imeshirikisha waandishi wa habari katika mpango huo wa kuboresha Elimu kwa sababu inatambua na kuthamini mchango wao katika Elimu. Pia ametumia fursa hiyo kuwaagiza Waandishi wa Habari Mkoa wa Pwani kutumia kalamu zao vizuri katika kuandika habari za mradi wa Shule Bora ambao ni mpango mkakati wa kutoa elimu bora kwa watoto wa madarasa ya awali na msingi.
Amesema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya waandishi wa habari na maafisa habari wa mkoa wa Pwani, wenye lengo la kuinua kiwango cha elimu kwa watanzania wote, kwa kuhakikisha kuna mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi wa jinsia zote.
Vile vile Bi Zuwena ameeleza kwamba mradi wa shule bora nchini una malengo mannne, la kwanza ni KUJIFUNZA (kuhakikisha watoto wanajifunza shuleni), la pili KUFUNDISHA (mfuko wa msaada wa UKAID utaunga mkono na kuimarisha kazi ya ufundishaji Tanzania), la tatu JUMUISHI (kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wakiwemo wenye uhitaji maalum mashuleni wanakuwa katika Mazingira salama na rafiki ili kuwawezesha kumaliza Elimu ya msingi na wanaendelea na Elimu ya Sekondari), na la nne KUJENGA MFUMO (mfuko wa UK Aids,utaunga mkono serikali na kuimarisha ili kupata au kuwa na thamani ya fedha katika utoaji wa Elimu katika ngazi zote Toka chini hadi Taifani).
Aidha, Zuwena amezielekeza Halmashauri za Mkoa wa Pwani kuhakikisha zinasimamia vizuri mradi huo ili uweze kuleta mafanikio makubwa hapa nchini hususani katika kuimarisha elimu kuanzia ngazi za chini kwa kusudi la kuwajengea msingi imara mpaka wanamaliza Elimu ya Sekondari.
Kwa upande wa Afisa Elimu Mkoa wa Pwani Sara Mlaki amesema kwamba kwa kipindi cha mwaka mmoja mradi wa Shule bora umekua na mafanikio makubwa changamoto nyingi zinazowakatisha masomo wanafunzi hususani wakike zimepungua kama vile ndoa za utotoni, mimba katika umri mdogo utoro n.k
Awali Afisa mahusiano wa mradi huo, Raymond Kanyambo, alifafanua kuwa Shule bora ni mradi wa Serikali unaolenga kuinua kiwango cha elimu katika ngazi ya awali na msingi nchini ambapo jumla ya Mikoa tisa nchini ukiwemo Mkoa wa Pwani, kigoma,Dodoma, Tanga, Mara, singida,Rukwa, simiyu na katavi zitanufaika.
Mpaka Mradi unakamilika utagharimu bajeti ya Paundi za kiingereza milioni 89 sawa TSh bilioni 271 ambapo program ikienda vizuri pia kuna uwekekano ukawa endelevu Kwa miaka mitatu tena endapo utafanya vizuri.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.