7.4.2024
Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa imetoa msaada kwa wahanga waliofikwa na Mafuriko yaliyoharibu mali mbalimbali kutokana na mvua zinazoendelea nchini katika baadhi ya Kata za wilaya ya Kibiti hususani mazao.
Akikabidhi msaada huo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Kamishna msaidizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu Ndg. Khamis Lutengo amesema baada ya kupokea taarifa na kutokana na hali halisi ilivyo wameona ni vema kuwapa mkono wa pole wakazi wa Kibiti ili kuweza kuokoa maisha ya watu waliothirika na Mafuriko hayo.
"Waziri Mkuu yuko pamoja nanyi wakazi wa Kibiti, ameona ni vema kuwashika mkono wa pole kuweza kuokoa watu waliathirika na Mafuriko haya" Alisema Kamishna huyo.
Msaada uliotolewa ni mahindi Tani 20, ndoo za maji 300 zenye ujazo wa lita 10, mablanketi 510, neti za mbu 540 mahema makubwa mawili, na Moja kwa Moja msaada huo utapelekwa katika Kata zote 5 ambazo wananchi wameathiriwa na Mafuriko.
Licha ya kupokea msaada huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Ndg. Rashid Mchatta amesema ngazi ya Mkoa inakwenda kuitisha kikao cha wadau kuona namna ya kuendelea kutoa michango na misaada mingine kadri itakavyowezekana ili kuweza kuwasaidia wananchi hivyo, ameiagiza kamati ya maafa (W) ya Kibiti kuweka kumbukumbu ya taarifa sahihi katika akaunti ya makusanyo pamoja na kuimarisha ulinzi wa msaada uliopokelewa ili ukafikie wahanga waliofikwa na madhira hayo ipasavyo.
Kwa upande wa Wilaya ya Kibiti Katibu Tawala wa Wilaya Bi. Maria Katemana akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia kitengo cha maafa kwa kujali na kuona umuhimu wa kutoa msaada huo kwa wahanga wa Mafuriko, hasa katika kipindi hiki chenye uhitaji sana. Pia Bi Katemana ameahidi kuwa watahakikisha wanasimamia vizuri zoezi la usambazaji wa msaada huo, ili iweze kuwafikia walengwa waliokusudiwa.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro amesema kamati ya maafa ngazi ya Wilaya imejipanga vizuri kuhakikisha wanawafikia walengwa wote katika Kata zote 5 za Mtunda, Msala, Maparoni, Kiongoroni na Mbuchi zilizokumbwa na Mafuriko kwa wakati huu.
Naye Diwani wa Kata ya Mtawanya Mhe. Malela Tokha baada ya kushuhudia mapokezi ya msaada huo, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. SSH kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na kudai kwamba anaamini msaada huo unakwenda kuwasaidia wananchi waliopatwa na maafa na kuwa faraja kwao katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.