01.06.2024
Afisa Elimu Mkoa wa Mbeya Mwl. Kiduma Mageni kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Dkt.Charles Msonde amewasilisha ujumbe Serikali namna inavyosikiliza na kutatua changamoto za Walimu nchini.
Ujumbe huu unakuja ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais kwa OR-Tamisemi kuhakikisha wanasikiliza na kutatua changamoto za walimu nchi nzima.
Akiwa Wilayani Kibiti Mwl. Mageni amesema katika utekelezaji wa agizo hilo tathmini iliyofanyika imebaini changamoto kubwa za Walimu ni upandaji wa madaraja, mabadiliko ya vyeo vya muundo baada ya kujiendeleza kielimu, malipo ya arrears, likizo na uwepo wa lugha zisizo na staha wanapofuatilia stahiki zao.
Kwa upande wa upandaji wa Madaraja nchini Mageni amesema zaidi ya Walimu 54,000 watarajie watapandishwa madaraja kwa mserereko na wengine 52,000 kupandishwa kawaida.
Hata hivyo Mageni amesema Tamisemi imeagiza kuhakikisha kuwa katika Mazingira ya kazi kunakuwa na nidhamu, haki, mshikamano na uwazi hususani katika malipo ya likizo, (DEO/MEK) kuidhinisha likizo mapema na kusimamia uwepo wa mpango wa uendaji likizo wa watumishi (Leave roster) kuanzia ngazi ya shule kwa kuwa na orodha kamili kabla ya kupelekwa utumishi.
Mbali na hayo Mageni amewasihi walimu kuendelea kuchapa kazi kwa bidii wakati Serikali ikiendelea kutatua changamoto zao huku ikitarajia mabadiliko makubwa kupitia maboresho yanayofanyika.
Mara baada ya kupokea ujumbe huo Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibiti Bi.Maria Katemana amesema ngazi ya Wilaya wameyapokea maelekezo yote na watahakikisha wanatekekeza kama walivyoelekezwa.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro amesema kupitia ujumbe huo Serikali itegemee kupata mabadiliko makubwa kutoka Wilaya ya Kibiti katika Idara ya Elimu.
Mwisho baadhi ya Walimu kwa niaba ya Walimu wote wamemshukuru Mjumbe huyo kwa ujumbe aliowafikishia wakisema Walimu wamepata Ari na nguvu mpya ya utendaji na kwamba wako imara wakiwa na utayari mkubwa wa kubadilika.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.