15.6.2024.
Ilipokuwa imesalia siku moja kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Shirika la msaada la Norway wakishirikiana na KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani waliadhimisha siku hiyo katika Kata ya Bungu Wilaya ya Kibiti kwa lengo ya kuwakumbuka watoto wa Kitongoji cha Soweto nchini Afika Kusini ambao waliouawa tarehe 16.6.1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.
Akitoa utambulisho Mratibu wa maadhimisho kutoka Shirika hilo la kidini Bi. Latifa Agustino amewasihi wazazi/walezi/jamii kuyafanya maadhimisho hayo kuwa maalum kwa ajili ya kuzungumzia changamoto na mahitaji ya watoto wa kiafrika kwa kutafakari na kuhakikisha watoto wanaishi katika mazingira salama.
Kaulimbiu ya mwaka 2024 inayosema “Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa maadili na stadi za kazi” ilinogeshwa zaidi na maigizo, shairi na ngonjera zenye jumbe mbalimbali kwa jamii kupitia maadhimisho hayo .
"Kaulimbiu hii imetoa wito kwa wazazi Serikali, Walezi na Wadau kutimiza wajibu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na makuzi ya mtoto ili aweze kukabiliana na changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili ili aweze kupata haki bila ubaguzi." Alisema Agatha.
Bi Agatha Lema ambaye ni Afisa Miradi aliendelea kusema kuwa maadhimisho hayo ni fursa ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa sera za kitaifa zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia stahiki zao kama vile Elimu, Afya, Maadili bora , Ulinzi pamoja na kukemea vitendo viovu wanavyofanyiwa watoto kama vile kubakwa, kulawitiwa, Vipigo, Matusi, Kutelekezwa n.k
Vile vile Afisa Miradi huyo amewataka wazazi kuwapatia watoto maarifa, kuwafundisha maadili mema, uadilifu, sambamba na kuwafundisha kufanya kazi mbalimbali bila kusahau kuwapa watoto fursa ya kusikilizwa haswa wanapoelezea changamoto zao.
Aidha Bi. Johnmary Richard akimwakilisha Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Kibiti amewataka wazazi na jamii kujitafakari kwa kina na kuchukua hatua madhubuti kutimiza wajibu wao kwa kuwalea watoto ipasavyo.
Naye Afisa Elimu Maalum Sekondari Wilaya ya Kibiti Mwl. Loisa Lambileki amewataka wazazi kutenga muda wa kuwa karibu na watoto ili kuweza kuwasikiliza na kubaini changamoto walizonazo sambamba na mahitaji yao.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.