NI KATIKA TAMASHA LA KUMBUKIZI YA BIBI TITI MOHAMED 2023.
1/12/2023.
Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti ni Moja ya Wilaya katika Mkoa wa Pwani iliyopokea TUZO katika hafla ya utoaji TUZO za UFANISI na UBORA wa ELIMU ( Bibi Titi Education performance Award) 2023 katika uwanja wa ujamaa Ikwiriri Wilayani Rufiji.
Katika hafla hiyo Kibiti imepokea TUZO na Cheti na kwa Halmashauri zinazosimamia upatikanaji wa chakula shuleni katika shule ya Msingi Ngalengwa.
Mara baada ya kupokea tuzo hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kibiti Bw.Hemed Magaro amewapongeza na kuwashukuru Maafisa elimu (Wilaya na kata),Walimu, Watendaji, Madiwani, Chama Tawala, Watumishi na viongozi wote huku akiwasihi kupitia TUZO hiyo ikawe chachu ya kuendelea kuhamasisha zaidi ili kila mtoto apate chakula shuleni.
Vilevile Afisa Elimu Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi (W) Mwl. Zakayo Mlenduka amesema tuzo ya shule ya Msingi Ngalengwa ni matokeo ya ushirikiano wa wazazi ,walimu na wanafunzi waliosimamia uanzishwaji wa kilimo cha mazao ya chakula shuleni ikiwa pia ni sehemu ya kuimarisha elimu ya kujitegemea yaani ( EK).
Hata hivyo Mwl. Mkuu wa shule ya Msingi Ngalengwa Bw. Elia Boaz Elia amesema kupokea TUZO hiyo katika shule yake imempa Ari zaidi ya kuongeza bidii na kuhakikisha watoto wanasoma kwa utulivu wakiwa wanapata chakula mwaka mzima.
"Nimefurahi kupata tuzo hii katika shule yangu, nitakwenda kuhamasisha zaidi walimu wenzangu wanafunzi na wazazi, kupitia TUZO hii ikawe mwendelezo wa kupata tuzo nyingine zaidi.
Awali Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde alisema wametoa TUZO za elimu kwa ajili ya kuongeza kasi ya utendaji kwa sababu baada ya Serikali kuja na mkakati wa kuboresha Elimu Tanzania, walimu kwa ujumla wamepambana kuhakikisha mkakati huo unakuwa na tayari wamekwishaona mabadiliko ambapo mpaka sasa 99% watoto wanajua KKK n.k.
Akizungumza na halaiki iliyojitokeza katika uwanja wa Ujamaa Ikwiriri Mgeni Rasmi ambaye ni Waziri wa OR TAMISEMI na Mbunge wa Rufiji Mhe. Mohammed Mchengerwa amesema ametoa tuzo kwa sababu ya utekelezaji mzuri unaoendelea kumuunga mkono Mhe. Rais na Bibi Titi ambaye alipenda sana elimu.
"Leo tunashuhudia matunda ya Bibi Titi, hususani katika masuala ya elimu , nyadhifa n.k kwa wanawake na mabinti, zamani haikuwa hivi, pongezi sana Rais Samia kwa kuliona hili." Alisema Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa amewapongeza walimu kwa kufanya kazi kwa juhudi kwani ufaulu wa wanafunzi katika ngazi ya wilaya wanaomaliza elimu ya Msingi umeongezeka kutoka wanafunzi 833,672 kwa mwaka 2022 hadi kuifikia wanafunzi 1,092,960 kwa mwaka 2023 sawa na 80.58% kwa ongezeko la wanafunzi 259, 288. wanaofaulu na kuendelea na elimu ya Sekondari.
Mhe. Mchengerwa aliendelea kusema kuwa kwa upande wa shule za Sekondari kidato Cha nne ufaulu wa wanafunzi umeongezeka kutoka wanafunzi 340,914 sawa na 80.65 % 2020 ikilinganishwa na wanafunzi 456,973 sawa na 87.79% 2022 ikiwa ni ongezeko la la 7.14 % ya ufaulu, vivyo hivyo kwa kidato cha sita ufaulu umeongezeka kutoka wanafunzi 93,136 sawa na 98.97 % mwaka 2022 hadi kuifikia 104,550 ambayo ni sawa na asilimia 99.23 mwaka 2023.
Aidha hali ya uandikishaji wa elimu ya Awali umeongezeka kutoka wanafunzi 1,233,305 mwaka 2020 hadi 1,315,074 mwaka 2022 ambapo hali ya udahili wa wanafunzi wa kidato Cha 1- 6 ukiongezeka pia kutoka wanafunzi 2,483,506 mwaka 2020 hadi kuifikia 377,355 mwaka 2023.
Mbali na hayo Waziri huyo kwa niaba ya Rais, amewapongeza Wakuu wa Mikoa kwa usimamizi mzuri wa kazi kwa kuzingatia maelekezo wanayopewa huku akiwasisitiza kuwasimamia vema Wakurugenzi wote kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao vizuri ikiwa ni pamoja na usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotakiwa kukamilika Disemba 30 mwaka huu.
"Wakuu wa Mikoa hongereni kwa usimamizi mzuri, Wakurugenzi ambao hamtakamilisha miradi Disemba 30, kila mmoja aanze kujitathmini mwenyewe kama anatosha" Alisema Mchengerwa.
"Wakurugenzi ambao watapatikana na ubadhilifu wa fedha za miradi maendeleo sitawafumbia macho.Alisema Waziri Mchengerwa.
Pia katika hafla hiyo Waziri Mchengerwa amewaagiza Makatibu Tawala Tanzania nzima kuhakikisha watumishi wote wanapata motisha,hususani walimu na kuwapandisha madaraja sambamba na malipo ya likizo kwa kila mtumishi kwani ni haki yao ya Msingi ili nao wawe na Ari kubwa ya utendaji kazi wa kila siku..
Akitoa shukrani baada ya Hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Antony Mtaka na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge, kwa nyakati tofauti wamesema wamepokea maelekezo yote waliyopewa wanakwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo katika kada zote zinazowahusu kiutawala. Pia wamemshukuru Rais wa awamu ya sita Mhe SSH kwa namna anavyotoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.