WAZAZI/JAMII WATAKIWA KUSIMAMIA MALEZI YA WATOTO.
Leo ni siku ya Mtoto wa Afrika, siku hii huadhimishwa barani Afrika ifikapo Juni 16 ya kila mwaka ikiwa ni utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Nchi huru za Afrika zenye dhamira ya kuwakumbuka Watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika kusini waliouawa kikatili na utawala wa ubaguzi wa rangi tarehe 16/06/1976.
Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo; “Zingatia usalama wa mtoto katika ulimwengu wa kidijitali” mwaka huu katika Mkoa wa Pwani kimkoa yameadhimishwa wilayani Kibiti Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ya maendeleo kama vile PASSADA, CAMFED, JICHO ANGAVU, INTERFAITH, HUDUMA YA WATOTO NA VIJANA KKKT n.k.
Katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amesema, jukumu la malezi ya watoto ni la wazazi na jamii kwa ujumla.
"Wazazi au walezi chunguzeni watoto wenu kabla na baada ya kutoka shule, ili kujua mazingira ya watoto, " Alisema Kanali Kolombo.
Kutokana na vitendo vya ukatili vinavyojiripotiwa, Kanali Kolombo amewataka wazazi kuacha tabia ya kumaliza changamoto hizo kijamii/kifamilia na badala yake kutoa taarifa mapema ili hatua stahiki zichukuliwe huku akitoa namba za kupiga bure kuripoti vitendo hivyo vinapotokea.
Katika maadhimisho hayo Afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Bi Grace Tete amesema kuwa wazazi wamekuwa chanzo kikubwa cha watoto kuharibikiwa, kwa kutojali kufuatilia mwenendo na makuzi ya watoto hususani katika matumizi ya simu katika umri mdogo.
Akisoma risala ya watoto kwa niaba ya watoto wenzake, Lilian Luhinda mwanafunzi shule ya msingi Kingwira amesema, Halmashauri ya wilaya Kibiti kupitia idara ya maendeleo ya Jamii, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto unaimarika, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa klabu za watoto mashuleni, masanduku ya maoni, utoaji wa vifaa vya shule kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, utoaji wa elimu ya ukatili dhidi ya watoto mashuleni, elimu ya lishe, na huduma za matibabu kwa wahanga wa ukatili.
Vilevile mtoto Lilian alisema, pamoja na jitihada zilizofanywa na Serikali bado kuna changamoto kubwa zinazowakabili watoto katika wilaya ya Kibiti, kwa asilimia kubwa Wazazi/ walezi wameoneka kuwa chanzo cha changamoto hizo kwa kushindwa kutoa huduma za msingi zinazohitajika kwa watoto (chakula, mavazi, malazi, elimu na mwongozo, huduma ya afya, kinga) na kusababisha watoto kushiriki katika shughuli hatarishi kwa ajili ya kujitafutia mahitaji.
Hata hivyo Lilian aliendelea kusema kuwa kukosekana kwa malezi sahihi kutoka kwa wazazi au walezi imekuwa sababu ya watoto wengi kukosa mwelekeo mzuri wa maisha na kujiingiza katika makundi hatarishi ambayo husababisha watoto kukabiliwa na matukio ya ukatili kama (ubakaji, vipigo, ajira kwa watoto, utelekezwaji, mimba za utotoni ) mambo yanayosababisha watoto kushindwa kutimiza ndoto zao.
Aidha kutokana na changamoto wanazopitia,watoto wameiomba serikali kuwachukulia hatua kali kisheria watu wote wanaofanya ukatili dhidi ya watoto ili iwe fundisho kwa watu wote. Pia wameiomba serikali kuendelea kutoa elimu ya ukatili na lishe mara kwa mara kwa wazazi na walezi katika shule za sekondari na msingi hasa katika shule ambazo zipo Delta au katika kata ambazo matukio mengi ya ukatili yameripotiwa (Kibiti, Bungu, Mjawa na Salale).
Licha ya ombi hilo pia watoto wameiomba Serikali kuwaelekeza Wazazi na walezi kufanya wajibu wao kikamilifu katika kuwalea watoto na kuwahudumia watoto wao huku wakiisihi Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki katika shule ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa chakula au uji ili kuwawezesha watoto kuwa na hali nzuri wakati wa masomo.
Afisa maendeleo ya jamii Mary Sanga Akisoma taarifa ya Wilaya ya kibiti kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji amesema katika Wilaya wamefanikiwa kuwajengea uwezo wazazi/walezi pamoja na Watoa huduma mbalimbali kwa watu wapatao 250 kwa kuwapa elimu ya Malezi na makuzi ya watoto wao. Vile vile Mary alisema, wamepokea mashauri mbalimbali yapatayo 508 ya ukatili wa kingono, ukatili wa kimwili, n.k.
"Katika kuhakikisha usalama wa watoto mpaka sasa mashauri 111 yamefikishwa katika vyombo vya dola (Polisi, Mahakamani) na watoto 315 wamepatiwa vifaa vya shule, huduma za afya, Elimu ya ukatili na ushauri nasihi" Alisema Mary.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.