9.5.2024
Taasisi za Aisha Sururu na Wiphas ambazo ziko chini ya mwamvuli wa Dini ya Kiislam zinazojishughulisha na masuala ya kijamii kwa pamoja zimeguswa na kuwapelekea misaada wahitaji walioathiriwa na Mafuriko Wilaya ya Kibiti ambayo yamedumu kwa takribani miezi miwili Sasa.
Mahitaji waliyopeleka ni mchele kg 200, unga wa ngano viroba 10 Vyenye ujazo wa kg 10, sembe kiroba kimoja chenye ujazo wa kg 25, sukari kg 25, sabuni ya mche boksi Moja, maharagwe kg 300 na mafurishi 6 ya nguo mchanganyiko zikiwepo za watoto na kinamama.
Mwanaidi Bakari ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya AISHA SURURU anasema wameguswa kuwasaidia wakazi wa Kibiti na ni moja ya utekelezaji wa majukumu yao hivyo wameona ni wakati sahihi kufika kuwafariji na kuwashika mkono walioathiriwa na Mafuriko.
Bi Mwanaidi pamoja na timu yake wamefikisha msaada huo shule ya msingi Kitundu ambapo wanafunzi wa madarasa ya mitihani kutoka shule zilizoathiriwa na mafuriko na wameweka kambi ili kuendelea na masomo yao.
"Sisi tunafanya kazi na jamii, tulionao hapa ni watoto wa darasa la 4 na la 7 wanaotarajiwa kufanya mtihani waliohamishwa kutoka kwenye makazi yao kutokana na shule zao kuzingirwa na maji, kwa kidogo hiki tulicholeta ni Imani yetu kitawasaidia wakiwa Kambini kwao ambapo wanaendelea na masomo" Alisema.
Vilevile Mwakilishi kutoka Taasisi ya Wiphas amesema pamoja na kwamba Taasisi zao ni za kidini, panapohitajika masuala ya kibinadamu hayaangalii Dini ndiyo maana leo jamii inashuhudia wamefika Kibiti.
Hata hivyo Shekhe aliyeambatana na msafara huo yeye aliwaasa watoto kusoma kwa uchungu na bidii ili waweze kufanikiwa na kufaulu katika masomo yao, kwani hata wao kuja kwao Kibiti wameguswa na kuona uchungu watoto kuhamishiwa katika Mazingira waliyozoea na kwenda kuishi katika kambi.
Aidha Kaimu Mkurugenzi ambaye ni Afisa Elimu Divisheni ya Awali na Msingi Mwl. Zakayo Mlenduka amezishukuru Taasisi hizo kuwapelekea msaada huo, akikiri kwamba umefika wakati muafaka kwani unakwenda kusaidia watoto ambao wamewekwa Kambini katika shule ya Msingi Kitundu kutoka maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na Mafuriko ili waweze kuendelea na masomo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.