Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Wilaya ya Kibiti imetoa siku 14 kwa wasimamizi wote wa Miradi ya maendeleo kuipitia upya mafaili ili kuhakikisha na kujiridhisha kuwa wamelipia kodi ya zuio ambayo ipo kisheria na huchangia kuongeza pato la Serikali.
Akizungumza katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, kamanda wa TAKUKURU Bi. Anna Shine amesema baada ya kufanya upembuzi yakinifu wamegundua kuna mapungufu katika ulipaji wa Kodi hiyo.
Vilevile amewataka wasimamizi wote wa MIRADI kuacha tabia ya kugushi mihutasari kwa madai ya ili fedha iweze kutoka haraka na kwa yeyote atakayepatikana na hatia Sheria itafuata mkondo wake kwasababu ni kesi isiyokuwa na faini zaidi ya kwenda jela.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo katika warsha hiyo aliwataka walengwa wote kutekeleza maelekezo yaliyotolewa ndani ya siku hizi 14 , na kwa atakayekiuka agizo Hilo basi Sheria ifanye kazi yake.
Mbali na hayo amesisitiza Mamlaka ya mapato kuhakikisha inafuatilia na kufanya tathmini ya miradi yote. Pia amesema kuna haja ya kutoa elimu kwa wazabuni ili kuweza kupunguza mivutano kati yao na wasimamizi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Ndg Denis Kitali amewasihi wataalam kusimama miongozo katika miradi yote huku akiahidi kusimamia na kufuatilia vema ili kuhakikisha thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali inaonekana.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.