22.07.2024
Shirika lisilo la kiserikali la TaTEDOSESO limetoa mafunzo muhimu ya utunzaji wa mazingira na uchomaji wa mkaa endelevu katika Kijiji cha Ngulakula na baadae wataendelea katika vijiji vingine Wilayani Kibiti.
Akitoa mafunzo hayo Mwezeshaji Shima Sago kutoka TaTEDOSESO amesema ili kuwa na uchomaji wa mkaa endelevu, wameanzisha utaratibu wa mashamba ya miti kwa ajili ya kupata malighafi ya kuchoma mkaa.
Mradi huo utasaaidia wachoma mkaa, wajasiriamali na wakulima wa kawaida kuanzisha mashamba ya miti ambapo watapewa miche bure pamoja na mafunzo ya kuyasimamia.
Katika Mafunzo hayo washiriki wamefundishwa uvunaji endelevu wa miti unaohusisha uchaguaji wa miti ya kuvuna (selective harvest), uvunaji wa kupumzisha maeneo, na matumizi ya Matanuru ya kisasa.
Vilevile Mratibu wa Mradi huo Afisa Maliasili Ndg. Dotto Mandago amesema mradi huo utasaaidia kuhifadhi misitu kwa wanajamii wa vijiji 10, na kupandisha mnyororo wa thamani kwenye uchakataji wa mazao ya misitu.
Akizungumzia Sheria na kanuni za misitu Afisa maliasili Ndg. Swalehe Kilindo amesema watatoa mwongozo wa njia bora za uchomaji wa mkaa kwa kutumia matanuru ya kisasa kama ambavyo Gn no. 417 kifingu cha 10 inavyoekekeza.
Nae Afisa nyuki kutoka wakala wa misitu Tanzania (TFS)-Kibiti Bi Paschalina Mwenesi amesema, katika kuhakikisha mradi unakuwa endelevu, watasimamia na kusaidia kwa karibu zaidi vikundi vya wafugaji wa nyuki vitakavyoanzishwa na TaTEDOSESO, sambamba na kusimamia rasilimali za misitu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Aidha washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru TaTEDOSESO kwa kuleta mafunzo hayo na wamesema wamejifunza vitu vingi ambavyo walikuwa hawavijui na zaidi wamepewa mbinu mpya ya utengenezaji wa tanuru la kisasa la kuchomea mkaa tofauti na walivyozoea.
Licha ya shukrani hizo washiriki hao wamesema Kupitia uanzishwaji wa mashamba ya miti ya kuzalisha malighafi ya kuzalisha mkaa watapata fursa ya kuongeza kipato kwani wapo watakaokuja kununua miti hiyo mashambani hivyo, watafanya biashara ya kuuza miti.
TaTEDOSESO limeendesha mafunzo hayo chini ya udhamini wa Umoja wa Ulaya kupitia Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lengo kubwa katika mradi huu ni kuimarisha utunzaji wa mazingira kwa kuacha kukata miti hovyo kwa kusimamia uchomaji wa mkaa kwa kutumia malighafi chache na kupata mkaa mwingi kwa matanuru ya kisasa n.k.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.