Askari wa MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), wameanza msako wa kuwatafuta na kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ambao huleta madhara kwa binadamu na kuzorotesha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo.
Zoezi hilo limefanyika katika Kata ya Mtunda ambapo Askari wenye silaha na ndoano (mitego) waliweka kambi ya siku mbili kwa kufanya doria na kuwafundisha baadhi ya wananchi namna ya kuwawinda Wanyama hao.
Wakiwa kijijini hapo wakati wa msako Askari hao wamefanikiwa kuwajeruhi mamba wanne katika Kata ya Mtunda kwa kuwapiga risasi ambazo zimewajeruhi na nimatarajio yao kuwa kwa tabia ya mamba kuoza akipata jeraha na kufa.
Akitoa mrejesho wa msako Kiongozi wa msafara, Askari Mhifadhi Humphrey Mkombo amesema licha ya kuwajeruhi mamba hao, wakiwa katika msako wamekutana na changamoto kwani Wanyama hao wapo kwa wengi tofauti na watu wanavyodhania, jambo linalofanya zoezi kuhitaji raslimali muda wa kutosha na vitendea kazi vya kuwadhibiti kwa wakati wasiweze kuendelea kuleta madhara kwa wananchi.
Vilevile Mkombo amesema wakiwa katika mto Longola walipokuwa wakifanya msako, wamegundua eneo lile kuna idadi kubwa ya mamba ambao wapo katika ukubwa wa aina mbili tofauti, aina ya kwanza ni mamba wakubwa wanaopenda kushambulia wakiwa ndani ya maji na aina ya pili ni mamba wembamba na warefu wenye mashambulizi makali na ya kushtukiza punde tu anapohisi Kuna binadamu ama mnyama yoyote wakufugwa kukanyaga mtoni (majini).
Aidha maaskari hao Humphrey Mkombo na Swalehe Msengi wamesema, kutokana na ukubwa watatizo, na tabia za mamba walio waona, wanaomba zoezi litekelezwe kwa kutumia vitendea kazi madhubuti na vikali ikiwa ni pamoja na uwepo wa tochi kubwa kwa ajili ya kumulikia ili kuwaona vizuri au kwa haraka.
Hata hivyo wamewapongeza wananchi kwa ushirikiano waliowaonyesha katika kipindi cha msako jambo lililochagiza kuongeza Ari ya utendaji.
Akitoa ufafanuzi wa zoezi hilo, Maafisa Uhifadhi Bi Zawadi Malunda na Bw.Sanjo Mafuru wamesema Kwa nyakati tofauti tofauti kuwa zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli zao za kila siku hususani katika maeneo yenye changamoto za Wanyama hao kwani jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na usalama.
Tulikuja na askari wetu na kuwaacha wakifanya msako, tunashukuru kwa ushirikiano wenu, hii itasaidia kufanikisha jambo hili kwani ninyi ndiyo wenyeji mnaojua maeneo yenye changamoto.
Akijibu maswali ya wanakijiji Bi Malunda amesema, katika kujali utu na watu wake Serikali imeliona hilo ndiyo maana wamefika maeneo yenye taarifa za matukio na sasa kazii meanza.
Vilevile Mhifadhi Mafuru amesema tayari Serikali imekwishaelekeza kuanzisha kwa vituo vitakavyokuwa na askari (wahifadhi) wataalamu kwa ajili ya kukabiliana na Wanyama ili kuweza kupunguza ukubwa wa tatizo au kumaliza kabisa kama moja ya njia ya kudumu ya kutatua changamoto hiyo.
Kutoka na na ukubwa watatizo,tayari wamekwishatoa muongozo wa maelekezo kupitia Kwa Ofisi ya Afisa Wanyamapori wa Wilaya na kuhakikisha uongozi wa Kijiji unaandaa vijana waaminifu wasiokuwa na jinai waliopitia mgambo, ili kuweza kupewa mafunzo waweze kufanya ulinzi shirikishi wa msako wa kukabiliana na wanyama hao.
"katika kuhakikisha tatizo hili linatokomezwa, tumeuagiza uongozi wa vijiji kuchagua vijana waadilifu waliopitia mafunzo ya mgambo, kujitolea waweze kufundishwa mbinu mbalimbali za kukabiliana na Wanyama hao". Walisema Wahifadhi hao.
"Tuwaondoe hofu, kazi imeanza tupo kazini,na mtaendelea kutuona vijijini mwenu mpaka tuhakikishe mambo yanakuwa sawa" .
Kuhusu kudhibitiwa kwa Wanyama wakali na waharibifu jambo la muhimu ni kutoa taarifa Kwa haraka na katika kujihami pale inapowezeka mwananchi anaruhusiwa kumthibiti mnyama huyo na kukabidhi nyara za serikali zilizopo na si vinginevyo.
Akifafanua utaratibu wa kulipa kifuta machozi kwa wahanga walioshambuliwa na Wanyama hao, Afisa WanyamaPori Wilaya ya Kibiti Ndg, Dotto Mandago ameweka wazi kuwa, kwa mtu aliyepoteza maisha fidia hulipwa 1,000,000, kwa mwenye ulemavu wakudumu hulipwa 500,000 na majeruhi hulipwa 200,000, kwa kufuata taratibu ba kanuni zilizowekwa na Serikali kuanzia ngazi ya kijiji. Aidha Mandago ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna inavyowajali wananchi wake kwa kuwalipa fidia, kwani ni nchi pekee Afrika na Afrika Mashariki ambayo hulipa fidia au kifuta machozi kwa wahanga waliopatwa na majanga.
Diwani wa Kata ya Mtunda Mhe. Omary Twanga ameishukuru TAWA kwa zoezi waliloanza huku akisisitiza zoezi hilo kuwa endelevu kwani tatizo lipo na watu wanapoteza maisha. Mbali na hilo pia amemshukuru Afisa Wanyamapori Wilaya ya kibiti Dotto Mandago kwa namna anavyojitoa kushirikiana na jamii ya watu wa Mtunda bila kujali muda wake,tunamshukuru sana.
Baadhi ya wananchi kwa niaba ya wananchi wenzao, wamesema mwanzo wa zoezi hilo kwao nifuraha, wamefarijikasana, huku wakiomba zoezi hilo kuendelea Ili kuweza kumaliza changamoto hiyo ya wanyamavwakali na waharibifu kwani wameshuhudia ndg zao wakipoteza maisha.
Ikumbukwe kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilianzishwa mwaka 2014 chini ya kifungu Cha 8 cha Sheria ya Kuhifadhi wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 ikiwa ni shirika la umma chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.