10.5.2024
Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori TAWA ni moja ya banda la maliasili lililotembelewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 Wilayani Kibiti wakiwa na lengo la kutoa elimu ya kujilinda na wanyama wakali na waharibifu hususani katika kipindi hiki cha mvua.
Katika banda Hilo Afisa Mhifadhi Bi. Zawadi Malunda Alisema katika kipindi hiki cha mvua kunakuwa na Mafuriko na Mafuriko hayo yanakuja na wanyama tofauti tofauti kutoka maeneo mbalimbli ambao wanaweza kuwa hatari kwa maisha ya binadamu
"Wakati wa mvua nyingi kama hizi zinazoendelea kunyesha nchini mara nyingi husababisha Mafuriko, wanyama wakali kama mamba kiboko huongezeka kwa asilimia kubwa na kusababisha maafa kwenye jamii kwa sababu wanakuwa katika harakati za kutafuta malisho baada ya kusombwa na maji kutoka kwenye maeneo waliyozoea.
Mhifadhi Malunda amewataka wanajamii kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu kandokando ya mikondo ya maji kwani ni chanzo cha kuharibu Mazingira kwa sababu wanapolima nyasi na miti zinazolinda udongo hupotea na matokeo yake ardhi kuwa nyepesi na maji kusambaa kwa urahisi.
Kwa muktadha huo Mhifadhi huyo amesema, kina cha maji hupungua na mchanga kujaa kwenye mito hivyo wanyama kama vile mamba hutoka kwenda kutafuta chakula kwenye maji mengi pindi Mafuriko yakitokea na katika mawindo ndipo hukutana na binadamu wakiwa katika shughuli zao za kila siku ama kwenye nyumba zao zikiwa zimezingirwa na maji lazima hivyo husababisha maafa.
Aidha, Mhifadhi Mafuru Sanjo ameelekeza kuwa namna ya kujihami na wanyama hao wakali na waharibifu kuwa kama mamba katika kipindi hiki ni pamoja na:
1. Kutembea Kwa Makundi (yaani zaidi ya mtu mmoja) Kwa kupita juu ya mito Kwa njia za madaraja)
2. Kutembea na vitu ama vifaa vyenye ncha Kali kama vile visu, mambo za miti iliyochongwa ili inapotokea uvamizi wake binadamu anaweza kujihami Kwa kumchoma machoni au tumboni ambako Kuna ngozi laini.
3. Kuacha kupita maeneo yenye maji na historia ya uvamizi wa mamba Kwa mifugo na binadamu nyakati za Usiku huku ukiwa umelewa pombe.
4. Ikiwezekana kunywesha mifugo kwa wafugaji kwenye majosho na visima badala ya kupeleka mifugo kwenye mabwawa ama mito yenye uwepo wa Mamba.
5. Kutumia kata au vichoteo vya maji vyenye urefu wa zaidi ya mita tano kwani Mamba anaweza kuvamia ndani ya urefu wa mita tano.
6. Kuacha mazoea ya kwenda mitoni ama ziwani kufua na kuoga, ikiwezekana Wananchi wakutumie maji ya mabomba,visima n.k yaliyoko majumbani kwao.
7. Kwa wakulima kuacha kulima mazao ndani ya mita 60 toka vyanzo vya maji huku wakiaswa kulima uzio/matuta/Kingo za kuzunguka mashamba yao ili kuzuia uvamizi rahisi wa mamba kwani wana miguu mifupi ambayo kwao ni vigumu kuruka kingo hizo kiurahisi.
8. Kutumia mitumbwi thabiti na imara (nyenzo za uvuvi imara) kwa wavuvi na kuacha kuzamia majini haswa maeneo yenye miamba na makorongo kwenye mikondo ya maji.
9. Kuacha matumizi ya uvuvi haramu wa kutumia mabomu ama vilipuzi ambavyo huaribu mazalia ya samaki ambayo mamba pia hutugemea kama sehemu ya malisho yao (Mamba ni carnivores ambaye ni predator)
10. Wafugaji wanaaswa pia kutochungia mifugo yao pembezoni mwa kingo za mito/maziwa ambapo mamba huyatumia kama sehemu za mazalio yao (Mamba huchimba na kutaga mayai yao kando kando ya mito/maziwa) na hivyo ni vema kujiepusha kuchungia mifugo ndani ya mita 60 toka vyanzo vya mito ilipo).
11. Kutoa taarifa mapema na kwa haraka kwa uongozi wa serikali ya Kijiji/Mtaa ama kwa Ofisi ya Afisa Wanyamapori wa wilaya husika pindi wanapoana uwepo wa Mamba ktk maeneo yao. Pia wanaweza kuwasiliana kwa namba za buree zisizo na tozo yoyote zilizotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA) kwa usaidizi wa haraka ambazo ni:0800110093 na 0800110098. Namba hizo ni mahususi Kanda ya Maalum ya DSM inayoshughulika na zoezi la kudhibiti Wanyamapori wakali na waharibifu kwa Mikoa ya PWANI,DSM na MOROGORO.
Mbali na banda la Tawa pia kulikuwa na banda la kongamano la vijana ambapo hapa kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa alishauri mabaraza ya Vijana kuanza katika ngazi ya Kata na kukutana kila robo ya mwaka kubadilishana mawazo jambo ambalo litaweza kuchuja na kuunda Baraza la Wilaya, kurejesha siku ya usafi ya Wilaya na kuweka Sheria Kali kama ilivyokuwa awali, kuunda vikundi vidogo vya uvuvi na kuviwezesha kupewa fursa pamoja na kutoa elimu kwa Vijana.
Pia Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa alitembelea banda la Uchaguzi ambapo alisisitiza jamii kuelimishwa kutambua umuhimu wa Uchaguzi na kujitokeza kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu nchini kama kaulimbiu ya Mwenge inavyoelekeza.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.