24.09.2924
Katika kusheherekea miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Kampuni ya mafuta ya Total Energies Duniani kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Leo septemba 24 wamekabidhi jumla ya madawati 130 katika Shule ya Msingi Jaribu mpakani na Shule ya Msingi Kitundu zilizopo Wilayani Kibiti ikiwa ni sehemu ya kurudisha shukrani kwenye jamii.
"Kwa hapa Tanzania Kampuni hii ilianzishwa mwaka 1969 na katika maadhimisho haya ya miaka 100 tumeona ni vema faida tuliyotengeneza tuilete Kibiti," Alisema Mpangile.
Akikabidhi madawati hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Sheria na Mahusiano kutoka Total Energies Bi. Getrude Mpangile amesema madawati 65 yatakwenda Kitundu na mengine 65 yatakwenda jaribu Mpakani. Pia akatumia fursa hiyo kuwasisitiza Wanafunzi wa shule hizo kusoma kwa bidii na kupandisha ufaulu ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao na kuendelea na masomo ya Sekondari mpaka elimu ya juu.
Vilevile Mpangile ameipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kuwa na miongozo mizuri waliojiwekea ya kutambua changamoto mashuleni na zinapotokea fursa kuelekeza penye uhitaji kama ambavyo wamewaelekeza TOTAL kupeleka msaada Kibiti.
Hata hivyo Bi Mpangile amesema licha ya kurudisha shukrani Kupitia Sekta ya elimu, kwa Total Energies Sekta hiyo ni kipaumbele hivyo wataendelea kusaidia kwa 90% kwani ni imani yao kupitia elimu watazalisha wasomi wengi kwenye vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TEA Bi. Mwanahamis Chambega ametoa Rai kwa walimu, wanafunzi na Wazazi kuhakikisha wanatunza vizuri madawati hayo ili yakadumu na kuendelea kusaidia wanafunzi wengine kwa miaka mingi zaidi.
Katika mapokezi hayo Afisa Elimu Divisheni ya Awali na Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mwl. Zakayo Mlenduka amewashukuru Total Energies kwa kuupa umuhimu uhitaji wa Kibiti bila kusahau TEA kwa kuusemea uhitaji huo kwa wadau hao wa maendeleo.
Aidha akipokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ameseishukuru Kampuni ya Total Energies kwa msaada waliotoa kwani unakwenda kupunguza changamoto iliyopo ya upungufu wa madawati huku akipongeza Mamlaka ya elimu Tanzania kwa kuwatafikia wafadhili hao.
"Kibiti tuna upungufu wa madawati 2767, kwa mapokezi ya madawati 130 uhitaji unaendelea kupungua ahsanteni sana, msisite kuja tena mtakapoguswa” Alisema Kolombo.
Nae Diwani wa Kata ya Mjawa Mhe. Ramadhani Chepa akatoa shukrani za Kata hiyo huku akiwapongeza TEA kwa kuwa msaada mkubwa lakini pia akawasisitiza Total Energies kuendelea kuwashika mkono kwani bado wanauhitaji mkubwa kwa upande wa madawati na hata kwa ujenzi pamoja na ukarabati wa shule hiyo ambayo ni kongwe.
Kwa nyakati tofauti Walimu Wakuu wa Shule hizo pamoja na wanafunzi wametoa shukrani zao za dhati kwa wafadhili hao wakiwaomba kutosita kwa kipindi kingine endapo watahitajika kwani msaada huo unakwenda kuwa chachu ya elimu licha ya changamoto zilizopo kama vile utoro, ufaulu, uchakavu wa majengo n.k
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.