30.5.2024
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amepokea na kukabidhi samani mbalimbali vikiwemo (viti, meza na madawati) kutoka kwa wadau wa Elimu Wilayani humo, ikiwa ni pamoja na fedha taslimu Sh. 1,850,000/=.
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya kupokea msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg.Hemed Magaro licha ya kuwapongeza wadau hao amesema mchango huo utawasaidia sana watoto ambao walikosa viti na madawati kwakuwa sasa watakaa vizuri darasani na kuongeza ari zaidi katika masomo yao.
Katika mapokezi na makabidhiano hayo, Kanali Kolombo amewapongeza wadau hao kwa umoja wao kwa kutimiza ahadi huku akisisitiza zoezi hilo kuwa endelevu kulingana na uhalisia wa uhitaji ili kuweza kupunguza kero ya upungufu wa samani katika shule mbalimbali ndani ya Wilaya.
"Leo nina furaha sana kuona matunda ya kikao cha wadau wa Elimu cha mwezi Februari kimeonekana kwa uhalisia". Alisema Kolombo.
"Tusivinjike moyo tuendelee kuchangia bado tuna uhitaji mkubwa katika shule zetu" Alisema.
Mbali na kukabidhi vifaa hivyo Kanali Kolombo ameiagiza pesa zilizopokelewa zikatengeneze samani ili lengo liliokusudiwa la kuwa na viti vya kutosha likatimie.
Awali akitoa taarifa ya waliochangia msaada huo Afisa Elimu Divisheni ya Awali na Msingi Mwl. Zakayo Mlenduka amefafanua kuwa wamependekeza kuwa, kati ya madawati 20, madawati 15 yanapelekwa shule ya Msingi Kitundu na 5 yanapelekwa shule ya Msingi kibwibwi wakati meza na viti 35 vinapelekwa shule ya Sekondari Mahege.
Habari picha ni matukio mbalimbali ya zoezi hilo la mapokezi na makabidhiano ya samani hizo kwa shule husika lililofanyika katika viunga vya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.