TAARIFA YA SHUGHULI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA RANCHI NDOGO KATIKA WILAYA YA KIBITI.
Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti ni moja ya Wilaya 7 za Mkoa wa Pwani ambazo zimeanza kutekeleza uanzishwaji wa ranchi ndogo za kufugia mifugo.
Ranchi ndogo ni eneo la ardhi lililoendelezwa kwa ajili ya kufugia na kuwekewa miundombinu ya mifugo na malisho.Mfumo huu umelenga kupunguza migogoro na kurejesha mahusiano ya kijamii baina ya wafugaji na wakulima ambayo yamelegalega kwa muda mrefu.
Hadi kufikia tarehe 25 Agosti, 2023 katika Wilaya ya Kibiti mpango huu umetekelezwa katika Kata tatu za Mjawa, Bungu na Mtunda zilizohusisha vijiji 4 vya Uchembe, Mtunda A, Muyuyu na Nyambili.
.
SHUGHULI ZILIZOTEKELEZWA NA MAFANIKIO YALIYOFIKIWA
Shughuli Na. 1: Utambuzi na upimaji wa maeneo ya malisho kwenye vitalu.
Jumla ya ekari za malisho zimetambuliwa katika Wilaya ya Kibiti ambapo katika kata ya Mjawa kwenye Kijiji cha uchembe ni ekari 1600 na vitalu 11, Kata ya Mtunda Kijiji cha Mtunda A ni ekari 6205 sawa na vitalu 50 na Kijiji cha Myuyu ni ekari 6,205 sawa na vitalu 50 na Kata ya Bungu Kijiji cha Nyambili ni ekari 1400 sawa na vitalu 15 vyenye ukubwa wa wastani wa ekari 125 Kila kimoja.
Shughuli Na. 2: Kuwapanga wafugaji na mifugo yao:
Katika maeneo yaliyopimwa tumewapanga jumla ya wafugaji 204 ambapo kati yao wafugaji 88 wamepangwa mmoja mmoja na
wafugaji 116 wamepangwa katika vikundi 14.
Idadi ya mifugo iliyopangwa ni 23,566 ambapo kati ya mifugo hiyo ng'ombe ni 23297, mbuzi ni 3,870 na kondoo ni 1,594 sawa na 45% ya lengo la kuipanga mifugo 52,784 inayochungwa kwa kuhamahama katika Wilaya Kibiti.
(A) VIGEZO VILIVYOTUMIKA KUWAPANGA WAFUGAJI NA MIFUGO YAO.
SIFA YA KUMILIKISHWA RANCHI
Zifuatazo ni taratibu za kufuata kupata ranchi (vitalu) kwa wafugaji kama ifuatavyo:-
1) Awe mfugaji anaetambulika Mkoa wa Pwani.
2) Awe tayari kuchangia gharama za utekelezaji wa mfumo.
3) Awe tayari kuomba kumilikishwa ardhi katika Kijiji atokacho au kitakachopendekezwa ikiwa ni pamoja na kulipa ada za maombi.
4) Awe tayari kijijini kulipa wajibu wa mfugaji jumla ya sh 175,000 kila mwaka, kulipa kodi ya ardhi 50,000 na vitalu 125,000 kupitia chama cha wafugaji.
5) Afanye Shughuli zinazoendana na ufugaji na si vinginevyo kama vile kufuga mifugo na kulima nyasi kwa ajili ya malisho.
Shughuli Na. 3: Kutoa elimu ya mahusiano mazuri baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Idadi ya wananchi waliopatiwa elimu ya mahusiano mazuri miongoni mwa watumiaji wa ardhi ni 697 na Viongozi 120 wa ngazi ya Tarafa, Kata na Vijiji.
(B) VIPAUMBELE VINAVYOTUMIKA KUPEWA VITALU
1) wafugaji wenye mifungo waliopo ndani ya eneo lililotengwa kwa ufugaji
2) Wafugaji wanaozunguka maeneo yaliyotengwa
3) mfugaji yeyote ambaye Yuko tayari kuingia kwenye mpango .
Shughuli Na. 4: UJENZI WA NYUMBA ZA WAHUDUMU WA MIFUGO NA MABOMA
Jumla ya wafugaji 22 sawa na 10% ya wafugaji waliopangwa wamejenga nyumba za kudumu za kuishi wahudumu na maboma ya mifugo yao.
CHANGAMOTO
1) Mgogoro wa mipaka ya vijiji
Uwepo wa migogoro ya mipaka katika baadhi ya vijiji ikiwemo mgogoro kati ya Kijiji cha Mtunda A na Muyuyu, imesababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa mpango.
UTATUZI
Migogoro husika ilitatuliwa kwa kufanya mikutano ya maridhiano miongoni mwa vijiji ambapo kwa pamoja walilidhia kuwa eneo husika litumike kufugia bila kuzingatia mipaka ya vijiji na kupewa jina la eneo la Jumuiya la kuchungia mifugo Mtunda A - Muyuyu.
2) Jamii ya kifugaji kuwa na utayari mdogo katika kushiriki kwenye mpango Ranchi ndogo
Hii ilitokana na wafugaji kuwa na mtazamo hasi kwa kuwa walizoea kufuga kiholela na Kwa kuhamahama.
Hali hiyo ilipelekea kuharibiwa kwa miundombinu inayowekwa kama vile alama za mipaka (bikoni), kutokuwa tayari kuchangia mpango huu na kutokuwa tayari kuwasilisha maombi katika Serikali za vijiji .
UFUMBUZI.
Changamoto hii imetatuliwa kwa kutoa elimu kupitia vikao na mikutano baina ya Wataalam, wafugaji, wakulima na Viongozi wa wafugaji.
3) UWEPO WA MAKUNDI YA WANANCHI WATUMIAJI WENGINE WA ARDHI TOFAUTI NA MATUMIZI YALIYOPANGWA.
Ilibainika kuwepo kwa jumla ya watumiaji wa ardhi 97 wanaotumia ardhi hiyo tofauti na matumizi yaliyopangwa kwa shughuli za uvuvi na kilimo.
UTATUZI
Hata hivyo changamoto hii ilitatuliwa kwa kuelimisha watumiaji hao kushiriki kutumia ardhi hiyo kwa shughuli zinazoendana na matumizi yaliyopangwa ambayo ni ufugaji.
MAPENDEKEZO
1) Kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa ranchi kwa wafugaji wote.
2) Wafugaji waliokwisha elimishwa kuendelea kuwapa elimu wachungaji wao kuacha kuharibu bikoni katika maeneo wanayochungia.
SHUKRANI.
Pongezi ziwaendee timu ya utekelezaji ikiongozwa na Daktari wa mifugo Mkoa wa Pwani Ramadhan Mwaiganju, Idara ya Mifugo wilayani, Kamati ya Ulinzi na Usalama (W) Wajumbe wa Serikali za vijiji, kitengo cha Mawasiliano Serikalini (w), Viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Wilaya, Tarafa, Kata na Vijiji Kwa kazi nzuri walioifanya kuhakikisha mpango wa ranchi unatekelezeka katika Kata za Mtunda, Mjawa na Bungu.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.