Mwenyekiti wa Jumuiya ya umoja wa Vijana Wilaya ya Kibiti (UVCCM) Amina Mkomboya leo tarehe 4.9 2023 ameanza ziara ya siku 11 ya kutembelea Kata za Wilaya ya kibiti kujionea shughuli zinazoendelea, changamoto zilizopo na kuona namna ya kuzitatua.
Akiwa katika Kata ya Bungu Bi Amina, amezindua tawi la kijiwe cha makao makuu ya UVCCM Kata ya Bungu A ambapo amesema amefarijika sana kushiriki katika tukio hilo muhimu.
Vilevile Bi Amina amewatembelea wanafunzi wa darasa la Saba shule ya msingi Bungu A na kutoa zawadi ya kalamu boksi 8 huku akiwasisitiza wanafunzi hao kuwa watulivu, kuzingatia waliyofundishwa na kufanya vizuri mitihani yao ya mwisho inayotarajiwa kufanyika septemba 13 na 14 mwaka huu.
"Tunatarajia mtafanya vizuri mitihani yenu na matokeo yenu kuwa mazuri someni kwa bidii " Alisema Amina.
Hata hivyo Mwenyekiti Amina amewashukuru wananchi wa Bungu kwa kumwamini na kumchagua, yuko tayari kuwatumikia muda na wakati wowote.
" Ahsanteni sana kwa kuniamini, niko tayari kuwatumikia, kuwapigania, na kuwasemea changamoto zenu zote, karibuni milango ya ofisi yangu iko wazi". Alisema Amina.
Katika ziara hiyo Katibu wa Jumuiya ya umoja wa vijana (UVCCM) Bw. Angelo Madale amewataka wanauvccm kuhuisha chama kwa kuzingatia maelekezo waliyopewa kwenye matawi ya ofisi zao, kwani uhai wa Chama ni pamoja na kufanya vikao, ziara ,kulipa ada na kuwa na kadi.
Hata hivyo amewapongeza Viongozi wa chama na Serikali ( Rais, Mbunge, na Diwani ) kwa namna wanavyohakikisha maendeleo yanapatikana Kata ya Bungu na Wilaya ya Kibiti Kwa ujumla.
Aidha ameagiza vijana kujitokeza kwa wingi kuomba nafasi za chipkizi zilizotangazwa ili waweze kushiriki na wenye sifa kuweza kugombea nafasi hizo.
Pia Katibu Madale amewataka wazazi na walezi wote kufuatilia mienendo ya watoto wao, wanapocheza, wanapoenda shule na kurudi ili kuimarisha maadili ambayo yamekuwa ni changamoto kubwa katika ulimwengu wa sasa na kuwasisitiza kusoma kwa bidii kwani elimu ndiyo urithi wa maisha yao.
Nao Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wilaya ya Kibiti Bw.Athman Mtoliya na Bi. Shamsa Mkulugo wamewataka wananchi na UVCCM kuendelea kuwaunga mkono Viongozi wao ili kuendelea kupata maendeleo mbalimbali yanayotekelezwa katika Wilaya ya Kibiti hususani Kata ya Bungu.
Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Kata ya Bungu Said Omary amesema ujio wa UVCCM Kata ya Bungu ni faraja kubwa huku akielekeza Jumuiya hiyo kuwa imara, kuzingatia yaliyozungumzwa na kuyatekeleza kwa vitendo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.