Tahere 17/02/2023 Wizara ya Afya chini ya ufadhili wa shirika la Afya Duniani (WHO) wamefanya uzinduzi wa kamati za uhamasishaji na uelimishaji juu ya magonjwa ya Mlipuko katika Ukumbi wa mikutano uliopo katika Jengo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
Katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo, ameitaka jamii kuchukua tahadhari za kukabiliana na magonjwa ya Mlipuko ikiwemo Cvid 19, Kipindupindu, Ebola, Kimeta na mengineyo kutokana na hatari kubwa ya kusababisha vifo.
Pia, ameipongeza Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa wanazozifanya za kukabiliana na magonjwa hayo hatari katika jamii.
Kanari Kolombo alisema magonjwa ya mlipuko yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika jamii, ambapo kwa Tanzania yalianza miaka mingi iliyopita hivyo kuna umuhimu wa kupata elimu kuyadhibiti kabla hayajatokea.
Pia aliipongeza na kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya inavyofanya jitihada za kudhibiti magonjwa hayo na kusema wataendelea kuunga mkono kwa kutoa elimu kwa wananchi wa Kibiti.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibiti Mohamed I. Mavura, alisema kuwa jamii ya Tanzania imepitia katika changamoto ya magonjwa mbalimbali ikiwemo Uviko 19, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwani yana athiri afya ya jamii na uchumi.
“Kwa kuwa Kibiti sio kisiwa, hatuna budi kujifunza mbinu na namna mbalimbali za kujikinga , kuwakinga na wengine Pamoja na kukabiliana na changamoto za mlipuko zinapojitokeza kwani mlipuko wa magonjwa unapojitokeza mahali kuna athari nyingi zikiwemo za kiuchumi”
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Kibiti Elizabeth Oming’o, alisema wamejipanga vyema kutekeleza kampeni hiyo ya kuelimisha jamii kukabiliana na magonjwa hayo ya mlipuko
"Tunapongeza Wizara ya Afya kwa kuja na mpango wa kutumia kamati ambayo inahusisha makundi mbalimbali hivyo wataisimamia vyema kupitia mipango yao," alisema Oming’o.
Kwa upande wake Mratibu wa Elimu ya Afya kwa umma kutoka Wizara ya Afya Dr. Johnson Mndeme alisema kwa awamu wa kwanza uzinduzi wa kamati hizi utafanyika kwa mikoa minne ambayo ni Tanga, Pwani, Geita na Manyara ambapo wanaendelea kuifikia mikoa mingine mikoa mingine.
Vilevile amesema Wizara ya Afya ikishirikiana na Shirika la Afya Duniani imeanzisha kamati za kutoa Elimu juu ya magonjwa ya milipuko kwa jamii, na kamati hizi zinazoundwa na wajumbe 45 zitakuwa katika ngazi zote kuanzia kata, wilaya Hadi mkoa. Aidha Wizara imefikia uamuzi huu baada ya kuona Serikali inatumia rasilimali fedha nyingi sana kupambana na magonjwa ya mlipuko yanapojitokeza hivyo ni vema jamii ikawa na desturi ya kupata Elimu kuliko kusubiri janga litokee.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.