Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge amewataka Wafanyakazi wa Mkoa huo kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza tija katika utendaji kazi na kuboresha maslahi yao wenyewe, kwani tija ikiwepo kutakuwa na ziada kubwa ambayo inaweza kufanya maboresho zaidi.
"Endeleeni kufanya kazi kwa bidii kwa sababu siku zote maslahi Bora hupatikana pakiwa na tija" Alisema.
Mhe. Kunenge amesema hayo alipokuwa katika maadhimisho ya sikukuu ya Mei Mosi ambayo Kimkoa yamefanyika katika Wilaya ya Kibiti yakiwa na Kauli mbiu isemayo Nyongeza ya mishahara ni Msingi wa mafao Bora na Kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha.
Akizungumzia changamoto mbalimbali zilizoziwasilishwa kupitia risala ya Wafanyakazi Mkuu huyo wa mkoa wa Pwani amewasihi Wafanyakazi kuendelea kuwa wavumilivu wakati wakisubiri matamko ya Viongozi wa Kitaifa kwani kuna masuala mengine ni ya kisera na tayari Serikali imekwishaanza kuyashughulikia ikiwa ni pamoja na suala la kikokotoo cha wastaafu, n.k
Hata hivyo amesema kuwa katika kukabiliana na changamoto zolizopo Mheshimiwa Rais anahangaika sana kuangalia namna gani anaongeza uwezo wa serikali kuboresha mazingira ya kazi nchini kama vile kuboresha mazingira ya shule ambazo watoto wanasoma, sekta ya afya na tayari ameahidi kuboresha makazi ya Wafanyakazi katika sekta ya elimu na afya na yote haya hufanyika kulingana na bajeti inayokuwepo.
Aidha kwa mazuri hayo amewataka Wafanyakazi kuzungumzia kazi nzuri anazofanya Rais Dkt Samia katika kuhudumia Wananchi nchini "mnapopata nafasi semeni mazuri yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye anawapenda na kuwajali Wafanyakazi nchini kwani anawahakikishia usalama na haki za Wafanyakazi kazini"
Mwisho Mkuu huyo wa Mkoa amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa Ndg. Rashid Mchatta kuhakikisha anachukua hatua kwa Taasisi au watu binafsi wanaokiuka maelekezo ya Serikali katika utendaji wa kazi.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph kolombo ameomba Serikali kuangalia namna ya kusaidia usafiri wa uhakika kwa Walimu wanaofundisha katika Shule za maeneo ya Kata za Delta ambako kutoka sehemu Moja kwenda nyingine hutumia mitumbwi au boti
Mbali na hayo pia katika maadhimisho hayo kumefanyika harambee ya kuchangia fedha mbalimbali kwaajili ya kupeleka misaada kwa Waathirika wa mafuriko wilayani Rufiji na Kibiti ambapo zaidi ya sh. milioni 4,400,000/- zilipatikana kwa ahadi na feda taslimu kwa ujumla.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.