Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Meja Edward Gowele ameagiza kukamatwa kwa wafugaji wote ambao mifugo yao huharibu mazao ya wakulima katika Kijiji cha Muyuyu Kata ya Mtunda ili Sheria iweza kufuata mkondo wake.
Meja Gowele amemuagiza Mkuu wa Polisi (OCD) Wilaya SSP H.F. Ramadhani kukamata mifugo yote inayozagaa mtaani na kuharibu mazao ya watu sambamba na kuwakamata wafugaji wa wanaoachia mifugo yao na kusababisha migogoro. Pia OCD ameagizwa kusimamia kikamilifu endapo ikitokea tena suala la udhalilishwaji wa wanawake huku akisisitiza waotendewa kutoa taarifa bila uwoga ikiwa ni pamoja na kutoa ushahidi mahakamani.
Hata hivyo amesema katika mikutano iliyopita alitoa maelekezo kwa wafugaji kujiandikisha ili wapewe maeneo yao (RANCHI) na kuyaendeleza huku akisisitiza kila upande kufuata taratibu na Sheria zilizopo kwa kuhakikisha eneo la kilimo kinafanyika kilimo na eneo la ufugaji ni malisho ya mifugo.
“Waliolima eneo la wafugaji acheni mara moja vivyo hivyo wanaofuga na kulisha eneo la wakulima hameni”alisema Gowele
Amebainisha hayo alipokuwa akijibu malalamiko ya wakulima ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara katika Kata hiyo ambayo ni kiungo kwa uzalishaji wa zao la ufuta na uchangiaji wa Mapato katika wilaya ya kibiti
Vilevile Katika kutatua kero hizo amemuagiza Mkurugenzi Mavura kuwa na mthamini wa mazao Wilayani ambaye atakuwa anatoa thamani ya uharibifu kwa ajili ya fidia.Pia amemuagiza Mwenyekiti wa Kijiji Hassan Mtwendwe kusimamia uundwaji mpya wa Kamati ya usuluhishi ambayo hutakiwa kuwa katika kila Kijiji ikiwa na wajumbe kutoka kwa wakulima na wafugaji kwa maelekezo ya kanuni na taratibu za kamati hiyo.
Kwa upande wa changamoto ya eneo la kilimo mwekezaji wa kilimo cha Mpunga Kata ya Mtunda Khamis kambagwa ameridhia agizo la Serikali,hivyo wakulima wajiandae kupata mbegu za kupanda kwani yeye atasafisha na kulima hekari 180 ndani ya siku 12.Pia ameomba kupewa heka moja kati ya 180 ambazo atalima ikiwa ni sehemu ya shamba darasa ambapo atatumia fursa hiyo kuwafundisha kilimo cha kisasa kinachosaidia kupata mazao mengi katika eneo dogo.
Aidha Mhe.Mkuu wa Wilaya amesema suala la changamoto ya mawasiliano ya mitandao ya simu amelibeba,kwa upande wa barabara upembuzi yakinifu umekwishafanyika huku akisisitiza kuwa upatikanaji wa haki mahakamani hutegemea na utayari wa ushahidi jambo ambalo ni changamoto kwa wakazi wengi wa maeneo hayo na hukusu mipaka shauri hilo linajadiliwa katika ngazi za juu Idara ya ardhi hivyo kuwe na subira wakati mgogoro huo unachakatwa.
Awali Diwani wa kata ya Mtunda Omary Twanga ,ameishukuru kamati ya ulinzi na usalama iliyoambatana na Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi pamoja na Wataalam wa ardhi kwa kuhudhuria mkutano huo wenye faraja kuhusu malalamiko ya wakulima wakisigana na wafugaji.pia amewataka wakazi wa Kijiji cha Muyuyu kuendelea kuwa wavumilivu na kuepuka kuchukua Sheria mkononi kwani malalamiko yao yanafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara .
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.