19.3.2024
Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji, Bodi ya Pamba Tanzania, Kampuni ya Pamba ya Rufiji (Rufiji cotton limited) kwa kushirikiana na Idara ya kilimo ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imefanya zoezi la uhamasishaji wa kilimo cha pamba katika vijiji 12 vya Kata 8 za wilaya ya Kibiti ambapo wameonekana kuhamasika.
Wakitoa taarifa ya zoezi hilo maafisa ugani wamesema, jumla wakulima 659 wamejisajili tayari kwa kuanza kilimo na kuchukua mbegu ambayo imekwisha sambazwa katika Kata 11 na mpaka sasa Tani 15 za mbegu ya pamba zimekwishapokelewa ambapo zinatarajiwa kupandwa katika hekari 1500 katika vijiji vyote.
Hayo yamejiri katika kikao kazi cha ufuatiliaji tathmini ya maendeleo ya kilimo cha pamba zoezi lililofanyika katika vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Kibiti ambapo maafisa ugani wametoa taarifa na kuja na maazimio mkakati kuweza kuimarisha kilimo hicho.
Hivyo katika kikao hicho wameazimia kila Afisa ngazi ya Kata, vijiji na vitongoji kuendelea kutoa elimu juu ya kilimo cha pamba, pembejeo kufikishwa mapema kwa wakulima na kuitumia kama ilivyoelekezwa kama viua wadudu na bomba zenye ubora. Maafisa ugani kuwezeshwa mafuta ili kuweza kuwafikia wakulima ,kuanzisha mashamba ya mfano pia kuwe na ufuatiliaji angalau kila mwezi kuhakikisha kilimo hicho kinafanyika ipasavyo Wilayani Kibiti n.k
Hata hivyo Meneja wa Bodi ya Pamba Kanda ya mashariki Ndg. Emmanuel Mwangulumba amesema licha ya kusambaza viuatilifu na mabomba watatoa maboza mawili, moja kwa Taasisi ya JKT Mkupuka na lingine kwa Gereza la Wilaya Mng'aru ili kuweza kurahisisha kilimo hicho.
Akizungumza kwa niaba ya Mwekezaji Bw. Lameck Mapalala amesema Kampuni ya Pamba Rufiji limited imedhamiria kushirikiana na wakulima kufufua kilimo cha Pamba Wilaya ya Kibiti, wanachohitaji ni kupewa takwimu za wakulima waliojisajili, kuna jumla ya hekari ngapi zitakazolimwa kila Kijiji ili waanze kazi haraka bila kupoteza muda.
Naye Balozi wa Pamba Tanzania Ndg. Agrey Mwanri amemsihi Mkuu wa Wilaya kusimamia kwa nguvu zote kurejesha kilimo cha zao la pamba Wilayani Kibiti kwani, wanatarajia kwa kila Kijiji kuzalisha Tani 210,000 baada ya kilimo kuanza rasmi.
Kuhusu masoko, Balozi wa Pamba Wilaya ya Kibiti na Diwani wa Kata ya Maparoni Mhe. Bakari Mpate amewaondoa hofu maafisa ugani akisisitiza kuzalisha pamba kwa wingi kwani masoko yapo na pamba ya Kibiti inatakiwa sokoni kulingana na ubora wake.
Aidha baada ya kupokea taarifa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewataka maafisa ugani wote kuhakikisha kiwango cha uzalishaji wa zao la pamba kinaendana na wingi wa mapokezi ya mbezu zilizopokelewa, huku akiahidi kuwa atahakikisha kilimo cha zao hilo kinaimarika na kuleta tija zaidi.
"Tumepokea Tani 15 za mbegu ya pamba ni nyingi, maafisa ugani mkasimamie vizuri kilimo hiki mazao yaendane na wingi wa mbegu tuliyoipokea," Alisema Kanali Kolombo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.