26.06.2024
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja. Edward Gowele amewasihi wakulima kuwa wavumilivu wakati Serikali inashughulikia malalamiko ya kuhusu Mfumo wa TMX ili wakulima hao waweze kupata haki zao.
Hayo yamejiri katika Mnada wa 3 wa zao la Ufuta Mkoani Pwani uliofanyika katika Wilaya ya Rufiji, ambapo katika mnada huo wakulima wote walikubali kuuza Ufuta wao kwa bei ya wastani wa sh. 3104.17 kwa kilo huku Tani 31 kutoka ghala la Misugusugu zikisalia kwa kukosa mnunuzi.
"Niwaombe mkawe wavumilivu wakati tunasubiri majibu ya Waziri mwenye dhamana ambaye tayari ameitisha kikao na viongozi wa Amcos Dodoma kujadili suala hili, baada ya kikao naamini tutapata majibu sahihi, Serikali yetu ni sikivu itasikia kilio chenu na kuja na majibu ya kutufurahisha". Alisema Meja. Gowele.
Aidha, Meja Gowele amewasisitiza wakulima wote kuhakikisha wanapeleka ufuta kwenye maghala na vyama vya Msingi wakati wakisubiri majibu ya Serikali.
Wakulima wa zao hilo, wameonekana wazi kutoridhika na kuulalamikia mfumo wa TMX ambao unaotumika kwa sasa katika uuzaji wa mazao mbalimbali nchini wakisema unawakwamisha na kuwaumiza kwani suala la mtandao ili kufungua na kuchakata bei ya mnada limekuwa likiwapotezea muda na bei ya mazao katika Mfumo huo imekuwa sio rafiki kwani imekuwa ndogo kuliko matarajio yao.
"Sisi mfumo huu tuliukataa tangu awali kwasababu tulijuwa utatuletea changamoto, tunaomba mturudishie sanduku tulilokwisha kuzoea wakati mkiimarisha mfumo huu, wakulima tunaumia" Walisema Wakulima hao waliofika Mnadani.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.