Kaimu Afisa Elimu divisheni ya Elimu ya awali na msingi Wilaya ya Kibiti Mwl. Costansia Assey amefungua mafunzo ya siku moja ya KKK kwa kanda ya Bungu, inayojumuisha kata za Bungu, Mlanzi na Mjawa yaliyofanyika katika shule ya msingi Songas yenye Lengo la kutoa maarifa ya uundaji wa zana na kuandaa mazingira mazuri ya ufundishaji kwa watoto.
Mafunzo hayo ni matokeo ya mafunzo kwa baadhi ya Walimu wawakilishi yaliyoandaliwa na Mradi wa Shule Bora unaofadhiliwa na shirika la UKAID kwa lengo la kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuinua kiwango cha Elimu jumuishi pamoja na kuweka mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi wote wakike kwa wa kiume katika shule za Serikali ya Tanzania.
Assey ambaye ni Mwalimu wa Elimu ya watu wazima na mlezi wa Elimu kata ya Bungu, amewataka walimu wote walioshiriki mafunzo hayo kuyapokea na kuyatumia kwa weledi ili yakalete mabadiliko kwa watoto pindi wafundishwapo darasani.
“Mafunzo haya ni ya msingi sana, husaidia kujenga uelewa wa jinsi ya kuwafundisha watoto ili wajue kusoma, kuhesabu na kuandika kwa haraka hivyo, pokeeni kwa moyo, na mafunzo haya yakawe chachu katika ufundishaji wenu. Na mara tuu baada ya mafunzo haya Idara ya Elimu inatarajia kuona tunapata mabadiliko chanya kwa upande wa KKK ”. Alisema Assey.
Katika kufikia malengo ya Watoto wote kujua KKK shuleni, nendeni mkawe na utaratibu wa kukutana na kubadilishana uzoefu wa zana na mbinu za kufundishia ili kuhakikisha watoto wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).Walimu wenzenu wamepewa mafunzo na baada ya kuelewa wamewafikishia maarifa waliyopata kwa kuwafundisha ili wote mkaelewe mbinu mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji.
Pia kutokana na vitendo vya ukatili kukithiri mashuleni na majumbani hususani vitendo vya ulawiti, Mwl Assey amewaagiza Walimu kuwa karibu na watoto ili kuweza kutambua na kujua mabadiliko yao kwa haraka kwani vitendo hivi vinarudisha nyuma maendeleo ya Watoto kitaaluma.
Vilevile Mwezeshaji wa mafunzo hayo Mwl Regina mbilinyi amesema mafunzo ya KKK yatasaidia kutokomeza tatizo la kutokujua kusoma ,kuandika na kuhesabu, pia kuongeza mbinu za ufundishaji na ujifunzaji na kuongeza ujuzi kwa walimu.
Mbilinyi amesema ili watoto wajue KKK wamejipanga kufundisha kwa bidii kwa kutumia zana mbalimbali walizojifunza, kutokomeza utoro na kuhakikisha watoto wanapenda shule na kufurahia masomo.
Aidha mafunzo yamehusisha Walimu Wakuu, Walimu wa Taaluma , Walimu wa darasa la awali, la kwanza, la pili na waratibu Elimu kata(MEK) ambao hawakupata bahati ya kudhudhuria mafunzo hayo chini ya mpango wa Shule Bora.
Naye mratibu wa elimu Kata ya Bungu Mohamed Mtuliakwako amewataka Walimu kutumia mafunzo hayo kuwa fursa kwa kujituma ili kuweza kupata mabadiliko ya haraka kwa watoto kwa kufanya kazi kwa bidii sambamba na uandaaji wa zana za ufundishaji.
“Tumejifunza tumeelewa, ndani ya miezi 3 tutafanya tathmini tujipime kama tumefika malengo”
Alisema Mtuliakwako huku akimwomba Afisa Elimu kupitia mafunzo hayo kuanzishwe mashindano ya kanda katika Wilaya ya Kibiti ili kuwe na hamasa ya ufundishaji na kuweza kufuta tatizo la Watoto kutokujua KKK.
Akizungumza kwa niaba ya Walimu walioshiriki mafunzo mwl. Kisa Anyagile Mwakobela wa shule ya msingi Pagae amewashukuru wawezeshaji kwa somo zuri kwani wamejifunza kuwa Mwalimu anatakiwa kutumia mbinu mbalimbali kufundisha, madarasa kuwa na Kona za ujifunzaji (zana) zitakazosaidia watoto kujenga uelewa wa kujifunza. Pia wamejifunza kuwapima watoto kwa kuzingatia mambo muhimu ili kutambua uelewa wa mtoto kabla na baada ya kumfundisha.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.