Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na programu ya shule bora Tanzania, imeanza kutoa mafunzo endelevu kwa walimu kazini (MEWAKA) kwa lengo la kusimamia utekelezaji wa moduli ya HISABATI iliyoboreshwa, kulingana na rasimu ya Mtaala mpya wa Elimu ya Msingi Wilayani Kibiti.
Shule bora ni mradi wa Serikali unaofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia mfuko wa UKAID unaolenga kuinua kiwango cha elimu ya Awali na Msingi nchini. Program ya Shule Bora inatekelezwa katika Mikoa Tisa Tanzania Bara kwa kwa Usimamizi wa Elimu ya Cambridge.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, ambaye ndiye mgeni rasmi aliyefungua mafunzo hayo, Bw. Hemed Magaro amewataka washiriki wa mafunzo ya HISABATI kusikiliza kwa makini ili waweze kuelewa wanayofundishwa kwani baada ya kupatiwa mafunzo hayo watatakiwa kwenda kufundisha wenzao ambao hawakupata nafasi ya kushiriki.
"Ninaamini kupitia mafunzo haya mtajengeka sana na kuimarika kiufundishaji mtakaporudi kwenye Kata zenu" Alisema Magaro.
Vilevile Bw. Magaro ameishukuru shule bora kwa namna walivyofikiria na kuwapatia mafunzo hayo kwakuwa kazi ambayo haina mafunzo UFANISI wake hudorora.
"Nikiri tu kwamba, kazi ambayo haina mafunzo UFANISI wake hupungua na kusababisha kudorora kwa mbinu za ufundishaji." Alisema Magaro.
Licha ya hayo Mkurugenzi Magaro alisema Serikali imetoa fedha nyingi sana kwenye Idara ya elimu na Afya, hivyo kada ya elimu walimu mna kazi ya kuhakikisha elimu inakuwa Bora na kiwango cha ufaulu kinaongezeka maradufu.
Mafunzo hayo yatakayoendeshwa kwa siku tatu yamehusisha walimu 16 wanaofundisha somo la HISABATI, Afisa anayeshughulikia programu ya shule bora Wilaya na Afisa Elimu Divisheni ya Awali na Msingi wa Wilaya.
Lengo la mafunzo haya ni kuimarisha umahiriwa walimu na viongozi wa Elimu katika kutumia mbinu shirikishi za ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Hisabati ili kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi wote.
Aidha baada ya mafunzo haya Walimu wa hisabati wanatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchanganua dhana mbalimbali za kihisabati, kufundisha kwa ufanisi na umahiri kwa kutumia mbinu za ufundishaji, kumudu stadi za upimaji endelevu ili kuboresha ufundishaji na kujenga stadi za utekelezaji wa MEWAKA katika ngazi ya shule.
Katika mafunzo hayo washiriki waliwezeshwa mada mbalimbali zikiwemo:
Kutambua umuhimu wa MEWAKA na Fursa zake katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.
Kutambua Changamoto katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa Hisabati.
Kubainisha uhusiano wa kimaudhui katika ya moduli ya MEWAKA na muhutasari wa somo la Hisabati kuanzia darasa la 5-7.
Kushirikishana uzoefu kuhusu ufundishaji na ujifunzaji wa Hisabati.
Kubainisha uhusiano wa kimaudhui katika ya moduli ya MEWAKA na muhutasari wa somo la Hisabati kuanzia darasa la 5-7.
Kutumia mbinu shirikishi za kufundishia na kujifunzia somo la Hisabati.
Kutumia zana za kufundishia na kujifunzia kwa mfano Jometri, Vipimo na Aljebra.
Kubainisha uhusiano wa kimaudhui katika ya moduli ya MEWAKA na muhutasari wa somo la Hisabati kuanzia darasa la 5-7.
Kwa habari picha ni matukio ya mafunzo ya Jana tarehe 7 Disemba yanayotarajiwa kuhitimishwa tarehe 9 Disemba 2023 katika ukumbi wa shule ya wavulama Kibiti.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.