12.06.2024
Shirika Uhifadhi wa ardhi oevu la Wetlands International limewezesha na kuendesha mafunzo ya kuongeza thamani kwenye bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wa maeneo ya delta Wilayani Kibiti.
Jumla ya wanajamii 20 wa vikundi vya ufugaji wa nyuki wamepatiwa mafunzo hayo wakiwemo viongozi (Afisa Maendeleo ya jamii wa Kata na Mtendaji wa Kata) kutoka katika vijiji vya Nyamisati, Kiomboni, Mfisini, Mchinga, Jaja na Ruma.
Mafunzo waliyopatiwa yamelenga kuongeza thamani kwenye bidhaa ili wajasiriamali hao waweze kuongeza kipato zaidi na kuweza kuzalisha bidhaa ambazo zitakuwa na ushindani katika soko la ndani na nje ya kibiti chini ya Mkufunzi Frank Bisheshara kutoka SIDO, ambayo ni elimu ya mnyororo wa thamani ambapo wamefundishwa kuongeza thamani ili kupata manufaa zaidi na namna ya kuendeleza biashara.
Pia wamefundishwa kuchakata asali,kutengeneza batiki ,upatikanaji wa masoko, namna ya kusikiliza wateja na kutoaji wa huduma kwa kutumia lugha nzuri yenye ukweli na uwazi chini ya Mkufunzi Chacha kutoka chuo cha ufugaji wa nyuki Tabora.
Katika mafunzo hayo Msimamizi wa mradi wa Wetlands international Ndg. Napoleon Frank amebainisha kuwa ni matumaini yao baada ya mafunzo washiriki wataweza kuzalisha zaidi bidhaa mbalimbali katika maeneo wanayotoka.
Licha ya hayo Ndg Frank amesema kazi kubwa ya Wetlands International ni kuhakikisha walengwa wanachangamkia fursa wanazotoa kwani zikitumika vizuri zitapunguza utegemezi na kuwaonyesha njia mbalimbali za kujikwamua na kuongeza mnyororo wa thamani kwenye bidhaa zao watakapokuwa wakizalisha.
"Tunaamini wakufunzi kutoka Sido na chuo cha nyuki Tabora wametoa mafunzo na mbinu sahihi zitakazoweza kuwasaidia wajasiriamali hawa kuongeza thamani" Alisema Frank.
Awali akifungua mafunzo hayo Mkuu wa kitengo cha Maendeleo ya jamii Wilaya ya Kibiti Ndg. Khamis mnubi amewataka wanajamii hao kutumia vizuri fursa hiyo iliyotolewa na wetlands international kwani wao ndiyo wanufaika wakubwa hivyo wanapaswa kusikiliza vizuri ili waweze kutoka na kitu kitakachowasaidia.
" Baada ya nyinyi kupatiwa mafunzo haya leo natarajia kukuta mabadiliko makubwa kupitia vikundi vyenu” alisema Bw. Mnubi.
Zaidi ya yote Mnubi amelipongeza Shirika la Wetland International kwa namna linavyokuwa karibu na jamii husika kwa kuwezesha mafunzo mbalimbali yenye tija.
Aidha kwa niaba ya washiriki wote wa mafunzo Bi. Salma Mwinga amesema kupitia mafunzo hayo na mengine mengi yatakayokuja wanaliahidi shirika hilo kuwa hawataliangusha watawawakilisha vyema kwa kutekeleza mafunzo kwa vitendo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.