NI KATIKA VIJIJI VYA NYAMISATI, MUYUYU NA MTUNDA A NA B.
Katika kutatua changamoto ya Wanyama wakali na waharibifu, MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kutoka Kanda maalum ya Dar es salaam, imewasili Wilaya ya Kibiti kutoa mafunzo kwa Wananchi juu ya namna ya kujilinda dhidi ya wanyama hao katika Kata ya Mtunda na SALALE wilayani humo kutokana na ukubwa wa tatizo.
Mafunzo hayo yaliyotolewa katika Kijiji cha Mtunda A na B, Muyuyu na Nyamisati ambao ni wahanga wa Wanyama waharibifu na wakali hususani mamba ambaye amekuwa akipoteza uhai wa wananchi wengi katika maeneo hayo na mengineyo.
"Tuko hapa kutoa mafunzo ya namna ya kujikinga na Wanyama hawa na hili ni zoezi endelevu, ili kuhakikisha wananchi wanaishi kwa usalama na kufanya shughuli zao za kiuchumi na kimaendeleo bila bughudha" Alisema Bi Zawadi Malunda.
Kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Nyamisati, Muyuyu na Mtunda A, na B Afisa Uhifadhi Bi Zawadi Malunda amesema shughuli za kibinadamu zinazoendelea kandokando ya vyanzo vya maji ndio chanzo cha Wanyama hao (Mamba, kiboko n.k) kufanya uharibifu wa mazingira hasa ya pembezoni mwa vyanzo vya maji (mito,mabwawa n.k) ukizingatia kuwa wanyamapori hao pembezoni mwa vyanzo vya maji ni sehemu yao ya malisho.
Licha ya hayo pia amesema, ukataji wa miti na mabadiliko ya tabia nchi huchangia kukauka kwa maji na kusababisha Wanyama hao kukosa makazi, malisho na kubaki wakitapatapa kuokoa uhai wao, pia Uvuvi haramu wa kutumia mabomu na sumu pia ukionekana ni chanzo kwani huua samaki wengi na kufanya ukosekanaji wa chakula katika Mito.
Hata hivyo Mhifadhi Malunda aliendelea kuwaelimisha wananchi kuwa, katika kujali utu wa mtu kuna kila sababu ya kuchukua tahadhali ikiwa ni pamoja na kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu kandokando ya mito, hususani maeneo yenye taarifa ya uwepo wa Wanyamapori hao wakali na waharibifu. Vilevile Mhifadhi Malunda amewataka wananchi kuhakikisha wanapovuka Mto au kufanya shughuli yeyote Chombo kiwe na mtu zaidi ya mmoja Ili kuweza kusaidiana pindi majanga/changamoto ya mashambulizi ya Mamba yanapotokea.
Kutokana na tabia ya mamba kufa Kwa haraka apatapo majeraha Kwa namna nyingine pia amewahimiza wananchi hao, kuwa na kitu chenye ncha Kali (kisu, panga, mambo, mkuki n.k) Ili wanapokuwa katika maji wakati Chombo kinapita kuchoma katika maji na kufanya mnyama huyo akimbie na kwenda mbali.
Aidha amesema tahadhali nyingine ni pamoja na kuhakikisha (kina mama) kuchota maji Kwa kutumia kichoteo chenye mti mrefu chenye umbali wa MITA 10 kwani Mamba ana uwezo wa kudaka Mtu ndani ya umbali wa MITA 5, Pia amewataka wakazi wa maeneo hayo kutoruhusu watoto kwenda kuoga mtoni peke yao. Huku akisisitiza kuwa njia nyingine za kujinasua kwa mamba ni kumtoboa macho yake, kutumia mitumbwi imara, Kuepuka kuchota maji ama kufua nguo kwenye eneo la maji yasiyoonyesha vizuri (maji yaliyochanganyika na vumbi/tope) ambapo Mamba huweza kujificha na kuvizia huku macho yao yakiwa na uwezo wa kuona vema tofauti na uwezo wetu binadamu (Mamba ana utando maalum kwenye macho unaomwezesha kuona vema akiwa majini)
Mbali na kutoa elimu ya kujihami Bi. Zawadi Malunda hakuacha kuwaelezea wananchi hao tabia za mamba kuwa ni mnyama mwenye akili na mjanja Sana ndiyo maana hufanikiwa katika mawindo yake Kwa urahisi, mifumo yake ya fahamu macho na ubongo wake viko juu, anauweza kuona akiwa ndani ya maji kutokana na utando alionao kwenye macho, mwenye uwezo wa kuhisi na kunusa akiwa mbali na tukio sambamba na kuhimili kukakaa ndani ya maji kwa dk 60 bila kuibuka baada ya kuvuta hewa ya oxygen, aliendelea kusema kuwa mnyama mamba hukimbia km 32 kwa saa akiwa majini na km 17 kwa saa akiwa Nchi kavu ukilinganisha na uwezo wabinadamu anayeweza kuogelea kwa kasi kubwa Duniani ya km 8.6 kwa saa.
Akielezea aina za mashambulizi ya mamba, Mhifadhi Mwandamizi! Ndg, Sanjo Mafuru amewasihi wananchi kuepuka kuishi kwa mazoea kwani mamba hushambulia kwa kushtukiza na pia ana uwezo wa kushambulia moja kwa moja akiwa majini kutokana na uwezo mkubwa alionao wa kuhisi na kunusa akiwa mbali.
"Msifanye mambo kwa mazoea kama vile kulewa pombe na kupita maeneo ya mito haswa majira ya usiku ndg zangu, suala hili halina uzoefu, lazima mchukue tahadhali zote (kutembea mkiwa wawili wawili ama zaidi, kutembea na mambo, visu/mapanga, tochi n.k) kabla na baada ya kuingia katika mito kufanya shughuli mbalimbali" Alisema Mafuru.
Njia nyingine ya kuchukua tahadhali ni Kwa wakulima kulima mazao yao nje ya MITA 60 toka kwenye chanzo cha maji Ili wanyapori hao wanapotoka majini waweze kukutana na malisho yao pasi na puguza. Huku wakizingatia kilimo cha uzio cha matuta ambacho huwazuia wanyamapori hao (Mamba/viboko) kupanda kwa uharisi kwani mikono na miguu yao ni mifupi
Hata hivyo bwana Mafuru alimaliza kwa kusema kwamba mbali na kujilinda, bado Uhifadhi wa Wanyamapori unatakiwa kuwa endelevu kwani ni muhimu katika masuala ya kiikolojia na kiuchumi kwasababu huchangia kuingiza pato la Taifa Serikalini.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kibiti Ndg, Zacharia Yahya Muhidini ameipongeza MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori TAWA kwa kutoa elimu, kwani changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu imekuwa ni tatizo kutokana na mashambulizi ya wanyama hao na kusababisha kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti kanali Joseph Kolombo ameisisitiza TAWA kuhakikisha inaunda vikundi vya ulinzi shirikishi na kuwajengea uwezo juu ya Wanyama hao, kwani vitasaidia kupunguza na kukabiliana na changamoto kwa wakati bila kusibiri Maafisa kutoka wilayani.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Mohamed Mavura katika kuhakikisha wanaokoa maisha ya watu na Mali zao dhidi ya wanyama wakali na waharibifu, ameitaka TAWA kuwa na mkakati maalum wa kudumu, bila kusibiri kuitwa hasa wakati wa miezi ya masika ambapo Wanyama hao husafirishwa na maji yaliyofurika na kumwagwa katika vyanzo mbalimbali vya maji.
Awali akiwakaribisha Wataalam hao, Afisa Wanyamapori Wilaya ya Kibiti Ndg, Dotto Mandago aliwahimiza wananchi hao kusikiliza kwa makini elimu wanayopewa na kutopuuza mafunzo wanayopewa, ili waweze kuzifanyia kazi kuweza kupekukana na Wanyama hao.
"Tumieni mafunzo haya mliyopewa msiyapuuze, yatasaidia kupunguza changamoto ya kushambuliwa na Wanyamapori wakali na waharibifu" Alisema Dotto.
"Tumekuja na askari tutawaacha hapa kuanza msako, ninaomba muwape ushirikiano" alisema Dotto.
Wakiwawakilisha wananchi wenzao baadhi ya wananchi baada ya mafunzo, wameishukuru TAWA na serikali kwa ujumla Kwa kusikia kilimo chao, na kuahidi kutumia elimu waliyoipata kujilind dhidi ya Wanyama waharibifu na wakali.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.