Wataalamu wa Kitengo cha Udhibiti taka na Usafi wa Mazingira pamoja na Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wilayani Kibiti wametembelea Klabu za Mazingira za Shule ya Sekondari Jaribu na Shule ya Sekondari Mjawa leo tarehe 20.02.2024 lengo likiwa ni kuwajengea uwezo Wanafunzi hao juu ya Usafi na Uhifadhi wa Mazingira.
Wataalamu hao wametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wanafunzi hao maana ya Mazingira, maana ya Takataka, aina za Takataka, njia za kupunguza Taka, umuhimu wa Mazingira, namna ya kuhifadhi Mazingira, sifa na malengo ya Klabu za mazingira mashuleni.
Pia Wataalamu hao waligawa miche 3,000 ya miti ya mbao na kivuli (miche 1,500 kwa kila shule) katika kuhakikisha Mazingira ya Shule hizo yanahifadhiwa kama wanavyokusudia.
Nao Wanafunzi wa Shule hizo walieleza hisia zao kuwa wamefurahia sana ujio wa Wataalamu hao kwani umewapa nguvu na hamasa ya kufanya shughuli zao za Mazingira kiukamilifu kwa kuwa leo wamewezeshwa kutambua umuhimu wao mashuleni.
Vilevile Wanaklabu hao wamewaomba Viongozi hao kuwawezesha kukutana na Klabu za Shule nyingine ili waweze kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo wa namna ya kufanya shughuli zao. Wakaenda mbali zaidi kwa kusema kuwa wanatamani pia kungekuwa na mashindano ya Utunzaji mazingira baina ya Shule zote Wilayani humo kila mwaka, jambo ambalo liliungwa mkono na Viongozi hao na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi maombi yao yote.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.