29.5. 2024.
Wakati Taifa likiwa kwenye mkakati wa kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati safi na kutunza Mazingira, shirika la Wetlands International limetoa mafunzo ya matumizi ya jiko banifu yanayotumia nishati ya Kuni na mkaa mchache kwa wakazi wanaoishi maeneo ya ukanda wa delta ya Rufiji ambako kuna misitu ya mikoko.
Mafunzo haya yamekuja kwa lengo la kuimarisha utunzaji wa Mazingira hususani uhifadhi wa misitu yenye miti ya mikoko Wilayani Kibiti ambayo ni delta pekee yenye mikoko aina 8 kati ya 10 inayopatikana Afrika Mashariki.
Akifungua na kufunga mafunzo hayo Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Bi. Diana Mahundi aliwasihi wananchi kuwa wasikivu, kuhakikisha wanaelewa wanachofundishwa kwa nadharia na vitendo ili wakatimize adhma ya wadhamini wa mafunzo hayo kwa kwenda kuwa wakufunzi wazuri katika jamii wanazotoka.
Wakiwa katika Kijiji cha Nyamisati ambako mafunzo yalifanyika kuanzia tarehe 22-24.5.2024 Mtendaji Kata wa Kata ya Salale Ndg. Haji Haji alitoa rai kwa washiriki wote, kuhakikisha kuwa kila mmoja anakuwa na jiko hilo ili ikawe chachu kwa jamii kupitia mafunzo waliyopatiwa.
Hata hivyo Mtendaji huyo alifafanua kwamba, mafunzo hayo yamehusisha wanajamii 15 kwa ujumla, yaani watu 3 toka kila kijiji (ambao ni mwananchi mmoja, fundi mmoja na Kiongozi mmoja).
"Tumechukua makundi haya katika kila Kijiji (watu 3) kwa lengo kuwashibisha mafunzo ipasavyo ili baada ya mafunzo wakawe wakufunzi kwa wanajamii wengine katika maeneo wanayotoka na kusambaza ujuzi huu".
Vilevile Ndg. James Kabute wa TFS alisema kupitia mafunzo hayo muhimu atafarijika sana iwapo wakati mwingine watakapotembelea maeneo ya delta watawakuta wanajamii hao wakiwa wanatumia majiko hayo ili thamani ya fedha iliyotumika kuendesha mafunzo hayo ionekane kwa uhalisia.
Aidha Msimamizi wa Shirika hilo Ndg. Frank Napolian amewashukuru wanajamii kwa kuitikia wito, kwani ni wazo walilokuwa nalo muda mrefu hivyo kwao ni furaha lengo limetekelezeka huku wakiamini kuwa ukataji wa miti ya mikoko utapungua kwa kiasi kikubwa kutokana na utegemezi wa nishati ya kuni na mkaa inayotumika kupikia.
"Leo kwetu ni faraja haya yalikuwa ni matamanio yetu kuhakikisha majiko banifu yanapatikana katika maeneo haya, ili kupunguza tatizo la ukataji wa miti ya mikoko ambayo ndiyo miti pekee inayopatikana katika uwanda wa delta".
Mara baada ya mafunzo kukamilika washiriki kutoka Vijiji vya Mfisini, Kiomboni Nyamisati na Mchinga kwa niaba ya wanajamii wamelipongeza Shirika la Wetlands International kwa kuja na njia mbadala kuwawezesha kupatiwa ujuzi huo kwani utawasaidia hata kupata kipato huku wakiahidi kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao katika Vijiji wanavyotoka na vingine pia.
Na katika hatua ya mwisho baada ya mafunzo ya vitendo, washiriki walitengeneza majiko banifu na kuanza kuyatumia ambapo wamesema majiko yaho ni mazuri na yanatumia kuni chache zaidi tofauti na yale waliozoea ya mafiga 3 na pia kwa uchache huo watapunguza ukataji wa mikoko na kutunza Mazingira.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.