Katika kuhakikisha utunzaji wa mikoko unaimarishwa Serikali iliandaa Mpango Mahususi wa Usimamizi wa Hifadhi za Mikoko mwaka 1990 ambao ulitumika nchini kote upande wa Tanzania bara. Mpango huo ulielekeza namna bora ya kusimamia na kutumia rasimali za mikoko miongoni mwa watanzania kwa kuainisha kanda nne ikiwa ni pamoja na kanda ya uhifadhi, kanda ya uvunaji, kanda ya upandaji na kanda ya uwekezaji mbalimbali kama vile ufugaji samaki, uzalishaji chumvi na uanzishaji wa miundombinu ya utalii ikolojia.
Kwa upande wa Wilaya ya Kibiti mpango huo ulifanyiwa mapitio kwa maelekezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu mwezi Septemba 2016 ambako matumizi ya rasilimali za mikoko yalisitishwa na Serikali. Mnamo mwaka 2018 hadi 2020 Serikali ilifanya tathimni upya ya rasimali za mikoko kwenye Hifadhi ya Mikoko ya wilaya ya Kibiti ambako shirika lisilo la kiserikali la Uhifadhi wa Ardhi-oevu Ulimwenguni lilitoa rasimali fedha za kuwezesha tathimini hiyo ambayo matokeo yake yaliwezesha Serikali kuandaa mpango mpya wa usimamizi wa mikoko ya wilaya hiyo kuanzia Julai 2021 hadi Julai 2026.
Mpango huo uliokuwa umeandaliwa kwa lugha ya kiingereza ulitafsiriwa kwa Kiswahili na wataalamu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa kushirikiana na Shirika hilo la Uhifadhi wa Ardhi-Oevu Ulimwenguni ambako tayari nakala 4,000 zimeandaliwa na kugawiwa kwa wanajamii wa Delta ya Mto Rufiji wilaya ya Kibiti kwenye mikutano ya uhamasishaji iliyofanyika katika vijiji vyote 19 vinavyozungukwa na mikoko. Mikutano hiyo ilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Mkuu wa wilaya Kanali Joseph Kolombo katika Kijiji cha Nyamisati ambaye aliwahimiza wanajamii wote kuzingatia maelekezo ya kisheria yaliyoko kwenye Mpango huo na kutunga sheria ndogondogo zitakazowezesha vijiji kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania-TFS.
Akimwakilisha Kamishina wa Uhifadhi TFS Prof. Dossantos Silayo Mhifadhi Mkuu Frank Sima alilishukuru shirika la Uhifadhi Ardhi-Oevu Ulimwenguni (Wetlands International) na pia kutoa rai kwa wanajamii kufuata maelekezo ya kikanuni yaliyooneshwa kwenye mpango huo wa Mwongozo wa Usimamizi na matumizi ya mikoko,na pia kuhamasisha kuhusu fursa ya kutunga Sheria ndogo za kusaidia utekelezaji katika ngazi ya Kijiji kwa vijiji vya wilaya hiyo ya Kibiti.
"Mwongozo wa usimamizi na matumizi endelevu wa misitu wa mikoko wa mwaka 2021 ibara ya 3 aya ya 1 kifungu namba g (3(1)(g) inasema, Serikali zote za Kijiji zinaruhusiwa kutunga Sheria ndogo zinazoweza kusimamia mikoko" Alisema Sima.
Awali Akimkaribisha Mgeni rasmi kuzindua vitabu hivyo Meneja wa TFS Wilaya ya Kibiti Mhifadhi Mkuu Devis Bernard Mlowe amesema vitabu hivyo vimeandaliwa kwa usimamizi wa karibu sana na TFS kwa kushirikiana na shirika la Wetland International ambao ni wadhamini wa uchapishaji wa vitabu hivyo, na endapo wananchi wakivisoma na kuvielewa watafanikiwa kwa kiasi kikubwa kutunza hifadhi ya mikoko.
Kabla ya Mgeni rasmi kuzindua vitabu hivyo Afisa Mradi wa Shirika la Hifadhi Ardhi-Oevu Tanzania Napoleon Frank amesema katika kutafuta mwarobaini wa kutunza hifadhi ya mikoko Pwani ya delta ya Rufiji waliona kuna haja ya ushirikishwaji wa jamii kupitia mpango huo ambao ulikuwa haujapitishwa tangu mwaka 1991.
Hata hivyo Napoleon amesema waliona ni vema kuwezesha kuandaa mpango huo wa kuzalisha vitabu vya Mpango wa Usimamizi wa Hifadhi ya Mikoko wa wilaya ya Kibiti kwa lugha ya kishwahili kwa manufaa ya watu wote, wakiamini wataweza kuvisoma na kuelewa kisha, kuanza kutunza vizuri rasimali za bahari (ikiwemo miti ya mikoko) katika ukanda wa Pwani.
Afisa Mradi huyo alibainisha kuwa kupitia vitabu hivyo watapata kupokea mawazo yenye tija kwenye jamii ya wakazi wanaozunguka hifadhi ya misitu hiyo ikiwa ni pamoja na mahitaji ya shughuli mbadala za kiuchumi na kijamii.
"Sisi WETLAND kwetu ni furaha, kwa sababu leo tumekamilisha ile nadharia tuliyokuwa tunawaza na kuona ina tija kwa wananchi na wadau kuwa itaongeza tija katika uhifadhi wa misitu ya mikoko." Alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti na Mgeni rasmi wa uzinduzi wa vitabu hivyo Kanali Joseph Kolombo amewapongeza TFS na WETLAND INTERNATIONAL kwa kuona umuhimu wa kuandaa Mpango na Mwongozo wa Usimamizi na Matumzi endelevu kwa lugha ya kiswahili.
"Nimefurahi kwa sababu lugha mliyoitumia kuandika mpango na mwongozo katika vitabu hivi ni lugha rafiki inayoeleweka kwenye jamii husika" Alisema Kanali Kolombo.
Kanali Kolombo amezishukuru Taasisi hizo kwa umoja wao kwa kukakaa pamoja kuandika Sheria hizo na kuvigawa vitabu hivyo katika vijiji vyote 19 vilivyopo ukanda wa mwambao wa Pwani wilayani humo, sasa anaamini wanakibiti watanufaika na kupata elimu ya utunzaji wa misitu ya mikoko na mazingira kwa ujumla kwa sababu watasoma na kusimuliana na mwisho kujenga uelewa wa nini kilichoandikwa.
Aidha, Kanali Kolombo amewaagiza wataalam hao kuhakikisha wanawapa semina wasimamizi wa Sheria hizo ngazi ya Kijiji ili waweze kuelewa na kutekeleza yaliyoandikwa ndani ya vitabu hivyo kipindi watakapokuwa wakielimisha wananchi.
Licha ya hayo Mkuu wa Wilaya aliwakumbusha wanajamii wote wa Kibiti kuendelea kuzingatia maelekezo ya Serikali kuhusu utaratibu uliowekwa ikiwa ni pamoja na masharti ya uvunaji katika kanda zilizoanishwa pekee kwa kufuata masharti ya uombaji na upatikanaji wa leseni, kutovua samaki kwenye maeneo yaliyoainishwa na sheria mbalimbali mtambuka, matumizi mazuri ya boti zilizotolewa na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuvua samaki kwenye maeneo ya kina kirefu cha Bahari, kuendeleza jitahada za upandaji mikoko kwenye maeneo ya wazi, na kuwa tayari kutumia fursa za utalii-ikolojia kwenye maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii katika ufukwe mrefu wa wilaya ya Kibiti wenye urefu wa km 65.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.