Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Bw. Hemed Magaro, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. SSH kwa kuijali Idara ya Afya ikiwepo Wilaya ya Kibiti na kuwapatia magari yanayokwenda kuongeza nguvu kazi katika kada hiyo.
Bw. Magaro amewaagiza watumishi wa Idara ya Afya kuhakikisha kuwa gari hilo linakuwa chachu katika kusimamia utoaji wa huduma Bora za Afya kwa wananchi wa Kibiti na usimamizi wa miradi ya Afya kwa ujumla.
Magari hayo yamekuja ikiwa ni mpango wa Serikali kuhakikisha shughuli za Idara ya Afya zinaimarika, ambapo jumla ya magari 520 kwaajili ya ufuatiliaji na tathmini yametolewa kwa Wilaya za Mikoa mbalimbali nchini.
Akimwakilisha Mhe. Rais Dkt. SSH ambaye ndiye alikuwa Mgeni rasmi katika kilele cha tamasha la Bibititi, tarehe 3 Disemba Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa amekabidhi magari 22 kwa Wilaya za Mikoa ya Dar re Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.
Waziri Majaliwa alikabidhi magari hayo mara tu alipowasili katika uwanja wa Ujamaa Ikwiriri - Rufiji baada ya kupokea taarifa ya kutoka kwa Waziri nchi TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, na kisha kutembelea mabanda ya maonyesho mbalimbali likiwemo banda la OR-TAMISEMI.
"Tunamshukuru Mhe. Rais kwa kutupatia magari haya, wito wangu, kila Halmashauri ikatumie magari hayo kwa malengo yaliyokusudiwa". Alisema Waziri Majaliwa.
Hata hivyo Waziri Mkuu Majaliwa amelitaka jeshi la Polisi kuwa na utaratibu wa Polisi kata kuhudumia shule na vyuo vyote katika Kata walizopo ili kuona maendeleo ya vitendo vya ukatili wa kijinsia licha ya kuwa idadi ya Polisi ni ndogo.
Pia amewaelekeza walimu wa shule za bweni kukagua na kuona kama kuna vitendo au viashiria vyovyote vya ukatili wa kijinsia na kuwasilisha taarifa haraka kwa Jeshi la Polisi.
Akihutubia maelfu ya watu waliojitikeza katika viwanja hivyo Mhe. Majaliwa amewapongeza wanarufiji na Mbunge wa Jimbo hilo kwa maandalizi mazuri huku akisisitiza kuwa maadhimisho hayo yaendane na ushupavu, uzalendo na ukombozi aliouonyesha Bibititi katika kutafuta maendeleo.
Waziri Mchengerwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji akitoa taarifa ya Tamasha Hilo mbele ya Waziri Mkuu amesema, katika kumuenzi Bibititi na kwa kutambua mchango wake wa Elimu, wamefanikiwa kutoa TUZO za UFANISI na UBORA wa ELIMU na kubwa zaidi likiwa ni kuweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Barabara ya Mohoro na kupewa jina la muasisi huyo.
Vilevile amesema shughuli zingine walizofanya katika Tamasha Hilo walitembelea shule na kufanya usafi wa mazingira , kupanda miti, kugawa vitanda shule ya Sekondari ya wasichana Bibititi, kugawa mitungi ya gesi kwa mama lishe, na kufanya Tamasha la utamaduni lililoshirikisha wasanii wa muziki na vikundi mbalimbali vya ngoma.
Licha ya shughuli hizo kwa upande wa utekelezaji wa ilani ya Chama Tawala wamegawa pikipiki na baiskeli kwa viongozi wa Chama kwenye Kata na Mashina sambamba na kufanya kikao maalum katika Ofisi hizo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.