Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Meja Edward Gowele akiwa ameambatana na Viongozi mbalimbali wa Wilaya wameutembelea umoja wa wakulima 311 wa kilimo cha mpunga wajulikanao kwa jina la MBAKIAMTURI wenye shamba la ukubwa wa Ekari 15550 katika Kijiji cha Mtunda A Kata ya Mtunda kujionea hali halisi ya uwekezaji katika eneo hilo ambao ni wa kipekee kabisa kuwahi kutokea katika ukanda wa Pwani ya kusini.
Wakiwa shambani hapo jopo la viongozi wa Wilaya lilijionea hali halisi ya uwekezaji wa wakulima hao waliojikita katika kilimo cha Mpunga , na katika kipindi hiki cha kiangazi walifanya jaribio la kilimo cha umwagiliaji ambapo tayari hekari 380 zimelimwa. Jaribio hilo lilikuwa na lengo la kuona kama wanaweza kufanikiwa kulima mara mbili kwa mwaka.
Vilevile Gowele ameziagiza kaya zilizoingia bila kibali katika eneo hilo la lililotengwa kwa ajili uwekezaji na zile zilizopewa kibali cha kuishi kwa muda huku wanafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo na ufugaji, kuhama maramoja katika eneo hilo ili kupisha shughuli za uwekezaji kwani muda wa kuishi huko umekwisha.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya MBAKIAMTURI Khamis Kambanga amesema,katika uwekezaji huo changamoto kubwa wanayokutana nayo ni ukosefu wa banio ,ambalo ni mashine ya kuzuia na kuruhusu maji Kusambazwa shambani kwani msimu huu walilima hekari 380 ambazo kwa sasa zimeanza kukauka baada ya ukosefu wa maji baada ya kuharibika kwa machine za kuvuta maji (water pump) walizokuwa wakizitumia awali.
Vilevile Kambaga amesema changamoto nyingine zinazowasumbua ni ukosefu wa barabara za kudumu jambo linalofanya usafiri kuwa mgumu na kusababisha gharama za usafirishaji wa mazao kuwa kubwa pia mazingira ya eneo la uwekezaji kuwa na mawasiliano ya kusuasua na ya kubahatisha hali inayofanya mawasiliano kuwa magumu mno.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya aliambatana na Katibu Tawala Milongo Sana, Mkurugenzi Mtendaji Mohamed Mavura pamoja na viongozi na wataalamu mbalimbali wa Wilaya hiyo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.