Mbunge wa Jimbo la kibiti Mhe. Twaha Mpembenue ameanza ziara ya siku 4 katika visiwa vya Kata ya Kiongoroni na Msala (delta) ikiwa ni sehemu ya kurudisha shukrani kwa wananchi kwa kumwamini na kumchagua na katika uchaguzi mkuu na kuwa mbunge halali wa Jimbo la Kibiti .
Katika ziara hiyo Mhe. Mbunge aliambatana na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali ambayo itahitimishwa katika Kata ya Msala na huko atakua mgeni rasmi katika mkesha wa sikukuu ya Maulid itakayofanyika tar 16 mwezi huu.
Akiwa katika Kata ya Kiongoroni Tarafa ya Mbwera Mhe. Mbunge amewashukuru wananchi na kuwaahidi kuwatumikia Kwa nguvu zake zote Kwa kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi .
Mpembenue ametoa mifuko 100 ya saruji Kwa ajili ya ujenzi wa shule shikizi katika kijiji cha King’ongo, mifuko 70 Kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya chama ya kata katika kijiji cha Jaja, mifuko 50 Kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi Kiongoroni na Mifuko 50 Kwa ajili ya shule shikizi Pombwe na kiasi cha shilingi laki moja na nusu (150,000/=) Pamoja na shilingi milioni moja (1,000,000/=) kwa ajili ya ukarabati mdogo wa Zahanati na shule ya msingi pombwe.
Pia ametoa sh. Laki 2 Kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wanaofanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne katika sekondari ya Mtanga delta na akaahidi kutoa bati 35 katika makao makuu ya Kata ya Kiongoroni Kwa ajili ya ukarabati wa nyumba ya Mwalimu huku akisisitiza wananchi Kuwa na tabia ya kujitolea katika shughuli za maendeleo.
Akijibu kero za wananchi katika Kata hiyo Mpembenue amewasihi wananchi kuendelea kuwa watulivu na kulinda amani hususani katika swala la wafugaji kwani jambo hilo linafanyiwa kazi katika ngazi ya Taifa na kuahidi kuwa changamoto zote amezibeba na anaendelea kuzifanyia kazi.
Vilevile Mbunge amemshukuru Mhe. Rais Samia Suhuhu Hassan Kwa namna anavyoendelea kutoa fedha za Maendeleo ya ujenzi shule barabara na miundombinu ya umeme ambapo mpaka sasa nguzo za umeme zimekwishafika katika Kata hiyo kwani kazi yake ni kusikiliza na kuwasilisha kero za wananchi wake na kuhakikisha zinatatuliwa.
Aidha amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kibiti Mohamed Mavura Kwa namna anavyoshirikiana nae kuhakikisha maendeleo yanapatikana huku akiwasihi wananchi kushirikiana nae bega Kwa bega Ili Kibiti iweze kusonga mbele.
Kwa nyakati tofauti Mwenyekiti wa Kijiji Cha Kiongoroni na Ruma wamemwomba Mhe.Mbunge kuwa na tabia ya kuwatembelea Ili kujenga Imani Kwa wananchi waliomchagua kwani kiu yao ilikuwa ni kuonana nae .
Nae Diwani wa Kata ya Kiongoroni Mhe. Muharami Tota, amesema amefurahishwa na kufarijika na ugeni wa Mhe. Mbunge na viongozi aliambatana nao, kwani umejibu maswali mengi aliyokua akiulizwa na wananchi wa Kata hiyo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.