21.08.2024
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo akiwa ameambatana na Katibu Tawala Bi. Maria Katemana amefanya ziara katika Kata ya Kiongoroni kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi sambamba na kukagua miradi ya maendeleo.
Akiwa katika Kitongoji cha King'ongo Kanali Kolombo amekagua ujenzi wa shule Shikizi King'ongo yenye jumla ya madarasa matatu na Ofisi moja ya walimu inayojengwa kwa mchango wa Mhe. Mbunge na nguvu za Wananchi ambapo ameahidi kuhakikisha Serikali inamalizia hatua iliyobakia.
Vilevile ametembelea shule ya Sekondari ya Mtanga Delta ambapo jengo la nyumba ya walimu iliharibiwa na kimbunga Hidaya pia alitembelea Zahanati ya Mtanga Delta na kubaini changamoto zilizopo kama ukosefu wa umeme, maji safi ya uhakika, makazi ya watumishi pamoja na uhitaji wa zahanati hiyo kurejeshwa katika hadhi yake ya kuwa Kituo cha Afya.
Pia Kanali Kolombo ametembelea Zahanati ya Ruma pamoja na Shule ya Msingi Ruma pamoja na Shule ya Msingi Kiongoroni iliyopo katika makao makuu ya Kata ambapo aliwataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii wakati changamoto walizonazo zikitafutiwa ufumbuzi na kisha akazungumza na Wananchi ili kusikiliza kero ama changamoto zilizopo kijijini hapo.
Akijibu kero za Wananchi Kanali Kolombo ameziagiza Taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya maji, umeme, vitambulisho vya Taifa ( NIDA ) na Vyeti vya vizazi na vifo (RITA) kuweka kambi katika maeneo hayo ili kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa wananchi hao huku akisisistiza mkandarasi wa Barabara kukamilisha Ujenzi wa Barabara ya kutoka Mtanga Delta mpaka Ruma kwa muda uliopangwa.
Kuhusu suala la Mifugo Kanali Kolombo amesema tayari wamekwishaanza Operesheni ambayo itakuwa endelevu huku akisisitiza kila mfugaji kuwa na kitalu cha kufugia Mifugo yake kwa kufuata utaratibu kwani itasaidia kumaliza migogoro ya mwingiliano wa malisho na mashamba ya wakulima.
Kwa upande wa elimu amewataka wakazi Kata ya Kiongoroni kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule na kuwataka walimu kuongeza jitihada za kufundisha kwa kushindanisha shule ili kwa kusudio la kupandisha ufaulu ambao umekuwa ni changamoto kubwa katika Wilaya hiyo.
Aidha ameahidi kuchangia Sh. 600,000 kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kitakachounganisha Kitongoji cha Bweni na Kijiji cha Kiongoroni na Sh. 200,000 kwa ajili ya ukamilishwaji wa shule ya Madrasa Kitongoji cha Bweni. Mbali na ahadi hizo amemuagiza Mkurugenzi kuhakikisha Ujenzi wa shule shikizi King'ongo unakamilika pamoja na kuwapelekea samani na ubao ili watoto wakasome katika Mazingira mazuri.
Mwisho Diwani wa Kata hiyo Mhe. Muharami Tota alimshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa ujio wake akisema kwao imekuwa ni siku ya kipekee yenye furaha kubwa katika historia ya Wanakiongoroni.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.